WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa ametoa siku mbili kwa Mkuu wa Idara ya Ardhi na
Miundombinu wa mkoa wa Rukwa pamoja na Ofisa Ardhi wa Manispaa ya Sumbawanga
kutatua matatizo ya ardhi yanayowakabili wakazi wa Manispaa hiyo.
“Ijumaa
kuanzia saa 3.00 asubuhi wenye kero za ardhi wote waende kwenye ukumbi wa
Manispaa mkuu wa idara atakuwa na watumishi wote na hapa mtasikilizwa kero zenu
na kupatiwa ufumbuzi. Nasiku hiyo hakuna kazi nyingine ni kusikiliza wananchi
tu,” alisema.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana jioni
(Jumatano, Agosti 24, 2016) wakati akizungumza na maelfu ya wakazi Mji
wa Sumbawanga waliojitokeza katika mkutano wa hadhara
uliofanyika kwenye kiwanja cha Mandela katika jimbo la Sumbawanga mjini ambapo aliwasisitiza
watendaji hao kuwasikiliza wananchi na kutatua kero zao.
Alisema
tangu alivyoanza ziara yake katika mikoa ya Rukwa na Katavi kila eneo alilopita
amekutana na wananchi wakiwa na mabango yanaeleza changamoto na hii inatokana
na viongozi wa mikoa hiyo kushindwa kutenga siku maalumu kwa ajili ya
kusikiliza kero hizo.
Waziri Mkuu alibainisha kwamba baadhi ya mikoa na halmashauri
mbalimbali nchini zimeshaanza utaratibu huo wa kutenga siku maalumu katika wiki
na kusikiliza matatizo yanayowakabili wananchi jambo ambalo limeanza kuonesha
mafanikio ya utatuzi wa kero hizo.
Awali
akizungumza katika mkutano huo mbunge wa jimbo la Sumbawanga Mjini Aeshi Hilaly
alisema wakazi wa Manispaa ya Sumbawanga wanakabiliwa na changamoto mbalimbali
ikiwemo ya migogoro mikubwa ya ardhi, hivyo alimuomba Waziri Mkuu kuwasaidia katika
kuipatia ufumbuzi.
Mbunge
huyo alisema migogoro hiyo ambayo imedumu kwa muda mrefu imewasababishia usumbufu
mkubwa wakazi wa jimbo hilo kukosa haki zao na muda mwingi wamekuwa wakiutumia
kufuatilia hatma ya ardhi yao bila ya mafanikio hivyo kurudi nyuma kimaendeleo.
Pia
mbunge huyo alimuomba Waziri Mkuu kuwaondolea zuio la kuuza mazao yao nje ya
nchi kwa sababu kitendo hicho kimesababisha kushuka bei ya mahindi na
kusababisha hasara kubwa kwa wakulima ambao wametumia gharama kubwa katika
kuandaa mashamba.
Akizungumzia
zuio hilo Waziri Mkuu alisema lengo la Serikali kuzuia uuzwaji wa mazao nje ni
kutaka kujiridhisha na uwepo wa chakula cha kutosha nchini ili kuepuka kukumbwa na baa la
njaa na kisha kwenda kuomba msaada kwenye nchi tuliowauzia.
Kuhusu suala la soko la mahindi Waziri Mkuu
alisema Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) watanunua
kwa bei ya soko na kwamba wataruhusiwa kuuza nje ya nchi baada ya Serikali
kujaza maghala yake huku wataalam wakimalizia kufanya tathmini ya hali ya
chakula nchini.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...