Waziri UmmyMwalimu.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,Waziri Ummy Mwalimu ameziagiza Hospitali zote za Rufaa nchini  ngazi ya Mikoa, Kanda na Hospitali ya Taifa Muhimbili kutoa Matibabu Bure kwa Wagonjwa wa Fistula.

Waziri Ummy aliyasema hayo mjini Tanga kwenye Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Bombo katika uzinduzi wa kambi ya matibabu ya Wagonjwa wa Fistula itakayodumu kwa kipindi cha wiki moja kuanzia tarehe 15 hadi 19 agosti,2016

Alisema  tatizo la Fistula limekuwa likiongezeka kila siku na waathirika wengi ni akina mama wa vijijini na wale wa  kipato cha chini ambao wanashindwa kupata huduma sahihi za afya ikiwemo kuchelewa kwenda kwenye vituo vya kutolea huduma za afya wakati wa kujifungua.

Takribani kina mama 2500 hadi 3000 hupata tatizo la ugonjwa  wa Fistula kila mwaka japo idadi hii ni ndogo sana kuliko hali halisi ilivyo kwa kuwa wagonjwa wengi hunyanyapaliwa na familia zao na jamii kwa ujumla.

"Serikali ya Awamu ya Tano imejikita zaidi katika kuwahudumia Wanyonge, kwa mamlaka niliyopewa natoa msamaha wa kulipia matibabu ya Fistula ili kuwapunguzia mateso wanawake hawa"."Kwa kuwa wenye tatizo la Fistula ni wanawake wa kipato cha chini na wa vijijini naziagiza Hospitali zote za Rufaa za Mikoa na Kanda kutoa Matibabu ya Fistula Bure kwa Wagonjwa watakaofika kutaka Huduma hizo."

Waziri Ummy alisema ili kuhakikisha huduma hizo zinatolewa ameziaagiza hospitali hizo kuandaa Kambi za Matibabu ya Fistula angalau mara moja kila mwaka na apatiwe Taarifa.

Aidha ,ameeleza kuwa kina mama wengi wenye tatizo la Fistula wamekuwa wakishindwa kufanya shughuli za uchumi kama biashara ndogo ndogo kwa kuwa ugonjwa huu ni wa aibu ambao hupelekea watu kunyanyapaliwa na jamii.

Akieleza hatua mbalimbali  zilizochukuliwa na serikali katika kukabiliana tatizo la ugonjwa huu ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa miundombinu kwa ajili ya huduma za ujauzito na uzazi, mafunzo ya huduma za dharura za uzazi kwa watoa huduma za afya pamoja na usimamizi shirikishi, uimarishaji wa ubora wa huduma za ujauzito na uzazi,kuimarisha upatikanaji wa dawa na vifaa tiba kwa ajili ya ujauzito na uzazi,kuimarisha mifumo ya rufaa na kuhakikisha huduma za dharura za uzazi zinapatikana hasa maeneo ya vijijini na wataalam waliobobea katika maeneo hayo.

"Utaratibu huu wa kushirikiana na wadau na marafiki zetu ni Mzuri, kwani unasaidia kuongeza ujuzi kwa wataalam wakiwa katika maeneo yao ya kazi. Pia,amewaomba wadau hao kuongeza wigo wa ushirikiano katika eneo la Afya ya Uzazi  ikiwemo matibabu ya Saratani ya Shingo ya Kizazi"alisema Waziri Ummy.

Kuhusu uhaba wa watumishi katika hospitali hiyo ya Rufaa,Waziri Ummy  ameahidi kupanga watumishi  wanaohitajika katika Hospitali za Rufaa za Mikoa pindi kibali cha ajira kitakapotoka,Vile vile  kutoa kipaumbele cha ufadhili wa masomo ya juu kwa madaktari watakaoomba kuchukuwa masomo yatakayowawezesha kubobea kwenye magonjwa ya akina mama na watoto.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Asha Mahita,alieleza kuwa hospitali ya Bombo ina changamoto ya kuwa na miundombinu chakavu, uhaba wa vifaa tiba na  watumishi kiasi ambacho wanashindwa kutoa huduma ya kutibu akina mama wenye tatizo la Fistula kwa kuwa hawana wataalam waliobobea katika maeneo hayo.

Naye Mwenyekiti wa The Sunshine Muslim Volunteers (SMV) Tanzania Dkt Juma Mwimbe alisema wameguswa na tatizo la fistula kwa kuwa linawakumba wanawake maskini na wa hali ya chini. Hivyo wataendelea kujitolea kwa kufanya kambi kama hizi kadri watakavyoweza ili waweze kuwafikia kina mama wengi zaidi hasa wa vijijini.

Kambi hii ya wiki moja inatarajia kuhudumia kina mama wapatao 100 kutoka Mikoa wa Tanga na Manyara ambapo wameweza kupatikana madaktari bingwa 7 kutoka nchi za Afrika Kusini, Pakistani, Australia na Uingereza.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...