Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kushoto)
akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani
Pangani mkoani Tanga. Waziri Muhongo yupo mkoani Tanga kwa ajili
ya kukagua miradi ya kusambaza umeme vijijini inayotekelezwa na
Wakala wa Nishati Vijijini (REA) pamoja na kuzungumza na wananchi.
Na Greyson Mwase, Pangani
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo amesema kuwa
Serikali ina mpango wa kusambaza nishati ya umeme katika wilaya
nzima ya Pangani na kuifanya kuwa wilaya ya mfano ndani ya kipindi
cha miaka miwili.
Profesa Muhongo aliyasema hayo alipokuwa akihutubia katika kijiji cha
Mkaramo kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga. Profesa Muhongo
yupo mkoani Tanga kwa ajili ya kukagua miradi ya usambazaji wa
umeme vijijini inayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Kabla ya kuwasili katika kijiji hicho msafara wa Profesa Muhongo
ulisimamishwa na wananchi wa kijiji cha Sakura kilichopo wilayani
Pangani mkoani Tanga waliokuwa na mabango wakiomba kupatiwa
umeme katika kijiji chao.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo akisisitiza jambo wakati alipokuwa akiwahutubia wakazi wa kijiji cha Mkaramo kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga (hawapo pichani).
Akizugumza kwa niaba ya wanakijiji wenzake, Boga Mbega alisema
kuwa kijiji hicho kimekuwa gizani kwa muda wa miaka mingi hali
inayopelekea uchumi katika kijiji hicho kudumaa.
Aliongeza kuwa kutokana na ukosefu wa umeme katika kijiji hicho
wamekuwa wakifuata huduma za jamii kama vile matibabu na maji
katika vijiji vya mbali na hivyo kuhisi kama wako kwenye kisiwa cha
giza.
Mara baada ya Waziri Muhongo kuwasili katika kijiji cha Mkaramo na
kuanza kuhutubia alisema kuwa kutokana na wilaya ya Pangani kuwa
nyuma kimaendeleo kuliko wilaya nyingine nchini, Serikali imepanga
mikakati ya kuhakikisha kuwa wilaya nzima ya Pangani pamoja na vijiji
vyake vyote inapata nishati ya umeme ndani ya kipindi cha miaka
miwili.
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainab Abdallah Issa (kushoto) akiwasilisha mahitaji ya umeme katika wilaya ya Pangani.
Akielezea malengo ya kuipa kipaumbele wilaya ya Pangani kwenye
mpango wa usambazaji wa umeme vijijini chini ya Wakala wa Nishati
Vijijini (REA), Profesa Muhongo alieleza kuwa ni kufuta umasikini
kupitia uboreshaji wa huduma za jamii kama shule, zahanati, pamoja na
kuzalisha ajira na kupunguza wimbi la vijana kukimbilia mjini kutafuta
ajira.
Alisema katika utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya tatu katika
wilaya ya Pangani, maeneo yatakayopewa kipaumbele cha kwanza ni
pamoja na shule, zahanati, vyuo, makanisani na misikitini.
Aliwataka wananchi wa wilaya ya Pangani kujiandaa na mradi huo kwa
kubuni fursa mbalimbali kama vile kuanzisha vikundi vidogo vidogo
kwa ajili ya kuanzisha viwanda, ukulima na ufugaji wa kisasa ili
kujipatia maendeleo.
Waziri wa Nishati na Madini (kulia) akipokea kero mbalimbali kutoka kwa wananchi wa kijiji cha Mkaramo.
Alifafanua kuwa ni wakati wa wakinamama wa wilaya ya Pangani
kuachana na matumizi ya kuni na kutumia majiko ya umeme na gesi.
Profesa Muhongo aliendelea kusema kuwa miradi ya umeme haihitaji
siasa na kuwataka wananchi kuweka nguvu zaidi kwenye uchumi kwa
kutumia nishati ya umeme badala ya kupoteza muda kwenye siasa.
Naye Mbunge wa Pangani Jumaa Hamidu Aweso (CCM) aliishukuru
serikali kwa kuipa kipaumbele wilaya ya Pangani na kusisitiza kuwa
wataanza kufanya uhamasishaji kwa wananchi wote wa Pangani .
Aliwataka wananchi kuachana na maandamano ya siasa na badala yake
waweke nguvu kwenye shughuli za kiuchumi zitakazowapatia
maendeleo.
Alisema kuwa mara baada ya umeme katika wilaya nzima ya Pangani
kupatikana, wawekezaji watajitokeza kuwekeza kwenye viwanda vya
korosho na kuongezeka mapato katika halmashauri ya Pangani.
Wananchi wa kijiji cha Sakula kilichopo wilayani Pangani mkoani Tanga wakionyesha mabango yenye jumbe tofauti mbele ya Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani) walipomsimamisha njiani kwa lengo la kuwasilisha kero mbalimbali wakati akielekea katika kijiji cha Mkaramo kwa ajili ya kuhutubia wananchi.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...