Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi |
Na May Simba-MAELEZO
Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi atakuwa mgeni rasmi katika
ufunguzi wa Bonanza la Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za
Serikali (SHIMIWI) ambalo litafanyika jijini Dar es salaam mwishoni mwa
wiki hii.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu Mkuu wa Shimiwi.
Bw. Moshi Makuka, bonanza hilo litafanyika tarehe 10, Septemba
mwaka huu katika uwanja wa Taifa (Uhuru) kuanzia saa 12:30 asubuhi.
“Bonanza litawashirikisha watumishi wote wa Serikali kutoka katika
Wizara, Idara zinazojitegemea na Wakala wa Serikali na Ofisi ya Mkuu
wa Mkoa Dar es Salam” alisema ndugu Makuka.
Aidha Bw. Makuka alisema kwamba bonanza hilo ni maandalizi ya
michezo ya Shimiwi ambayo yamepangwa kufanyika Mkoani Dodoma
kuanzia tarehe 14 mpaka 27 Octoba mwaka huu.
Michezo ya mwaka huu ina lengo la kuunga mkono agizo la Mhe.Rais
wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli la
kuhamishia Makao Makuu yake mkoani Dodoma.
Mbali na hayo Bw. Makuka alisema michezo hiyo itawapa fursa
watumishi wa umma kufahamu mazingira na kufanya maandalizi
muhimu kwa ajili ya kuhamia mkoani humo
Bw. Makuka aliongeza kwamba walipanga michezo hiyo kuanza Octoba
14 ili kuadhimisha kumbukumbu muhimu ya kifo cha Baba wa Taifa
Hayati Mwl. Julius Nyerere na kuenzi agizo lake la Serikali kuhamia
Dodoma linalotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano.
“Michezo ya mwaka huu itaanza na ibada maalumu ya kumuombea
Baba wa Taifa na kumtakia afya njema Mhe. Rais Dkt. John Magufuli
sanjari na kushiriki upandaji miti katika maeneo yatakayopendekezwa
na Serikali ya mkoa”aliongezaBw. Makuka.
Michezo ya Shimiwi hufanyika kila mwaka kwa lengo la kuwaunganisha
wafanyakazi wote na kuimarisha afya zao ili kuepuka maradhi ya mara
kwa mara.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...