Benki ya TIB Corporate imeingia mkataba wa ubia na Benki ya Posta Tanzania (TPB) utaoiwezesha benki hiyo (TIB Corporate) kutoa huduma zake kupitia matawi makubwa na madogo zaidi ya 60 ya benki ya Posta yaliyopo kote nchini.

Akizungumza wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana , Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate Bw Frank Nyabundege alisema ushirikiano huo wa kimkakati unalenga kuwaongezea wigo wa kibiashara wateja wake kupitia zaidi ya matawi makubwa 30 na mengine madogo 30 ya TPB yaliyopo kote nchini.

"Ushirikiano baina yetu unakwenda sambamba na mtazamo na malengo ya benki yetu kuhakikisha tunawafikia wateja kwa ukaribu kadiri tuwezavyo. Umuhimu wa aina hii ya ushirikiano unaonekana kuwa na tija zaidi kwa sasa kwa kuwa nchi yetu inaelekea kujikita kwenye uchumi wa viwanda hivyo kama taasisi ya fedha tunawajibu wa kuwa karibu zaidi na wateja wetu,’’ alisema Bw Nyabundege.

Alisema ushirikiano huo utahusisha huduma zote muhimu zinazotolewa na benki yake sambamba na kuhakikisha suala la usalama katika mihamala ya wateja wa benki hizo kwa kuwa masuala ya uhamisho wa fedha hayatahusisha ubebaji wa fedha kwenye mifuko huku pia suala la kutunza siri za wateja likizingatiwa zaidi.

“Hivyo basi iwapo mteja wetu ataweka pesa zake kupitia benki ya Posta, kiasi hicho cha pesa kitaingia kwenye akaunti yake benki ya TIB Corporate mara moja,’’ alibainisha. Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa TPB, Bw Sabasaba Moshingi, alipongeza ushirikiano huo huku akibainisha kwamba wateja wa benki yake pia watanufaika na mpango huo.

"Baadhi ya wateja wetu wamekuwa wakifanya biashara na wenzao wenye akaunti za benki ya TIB Corporate hivyo kupitia ushirikiano huu wateja wetu watakuwa wamerahisishiwa shughuli zao za kibiashara. Kwa sasa benki yetu ina matawi makubwa zaidi ya 30 na mengine madogo 30 kote nchini, hivyo ni wazi kwamba ushirikiano huu una tija kubwa katika kipindi hiki cha kujenga Tanzania ya viwanda ,’’ alibainisha.

Zaidi Bw Moshingi alitoa wito kwa wateja wa benki zote mbili kuutumia vyema ushirikiano huo ili uwe na tija zaidi katika shughuli zao za kibiashara.  
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate Bw Frank Nyabundege (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (TPB) Bw Sabasaba Moshingi (kulia) wakibadilishana mkataba wa ubia utaoiwezesha benki ya TIB Corporate kutoa huduma zake kupitia matawi 32 ya benki ya Posta Tanzania yaliyopo kote nchini wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana. Wanaoshuhudia ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya TIB, Bw Jaffer Machano (wa kwanza kulia),Mkurugenzi wa Teknolojia na Uendeshaji wa TPB Bw Jema Msuya (katikati) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa benki ya TIB Rasilimali, Bi Antoinette Tesha-Ntlemo (wa kwanza kushoto)
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya TIB Corporate Bw Frank Nyabundege (kushoto) na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Posta Tanzania (TPB) Bw Sabasaba Moshingi (kulia) wakibadilishana mkataba wa ubia utaoiwezesha benki ya TIB Corporate kutoa huduma zake kupitia matawi makubwa na madogo zaidi ya 60 ya benki ya Posta Tanzania yaliyopo kote nchini wakati wa hafla fupi ya kusaini makubaliano hayo iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Maendeleo ya TIB, Bw Charles Singili (wa pili kulia), akizungumza wakati wa hafla hiyo.
Mkurugenzi Mkuu wa benki ya TIB Rasilimali, Bi Antoinette Tesha-Ntlemo ( kushoto) akizungumza wakati wa hafla hiyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...