Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani (mbele) akielezea juhudi za Serikali kwa Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) za kuboresha huduma za upatikanaji wa nishati ya umeme. Wengine katika picha ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird na ujumbe kutoka Benki ya Dunia pamoja na Viongozi Waandamizi kutoka Wizara ya Nishati na Madini na Taasisi zake.
 Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia, Bella Bird na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia wakimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) katika kikao hicho kilichofanyika katika Ukumbi wa Wizara hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (kushoto) akimsikiliza Naibu Waziri wa Nishati na Madini Dkt. Medard Kalemani (hayupo picha) wakati walipokutana na Ujumbe wa Benki ya Dunia  ili kufahamu Serikali imejipanga vipi katika kuendelea kuboresha huduma za Umeme na wengine katika picha ni Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Nishati Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili), Kaimu Kamishna wa Nishati, James Andilile (wa tatu), Kaimu Kamishna wa Umeme, Innocent Luoga (wa nne), Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Nchini (Tanesco) Mhandisi Felchesmi Mramba (wa tano) na Kaimu Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Boniface Gissima Nyamohanga. 

Na Rhoda James 
IMEELEZWA kuwa uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia na maji umechangia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama ya uzalishaji wa umeme nchini.

Hayo yameelezwa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Dkt. Medard Kalemani wakati wa kikao chake na Ujumbe wa Benki ya Dunia na baadhi ya watendaji wa Wizara na Taasisi zake.
Akijibu baadhi ya maswali yaliyoulizwa na Ujumbe huo, Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali imepunguza gharama ya uzalishaji wa umeme baada ya kukamilisha ujenzi wa mitambo ya kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia na baada ya kukamilika kwa bomba la kusafirishia Gesi asilia kutoka Mtwara na Lindi hadi Dar es Salaam.

Aliongeza kuwa hivi sasa uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme nchini umeongezeka hadi MW 1,357.69 ambapo MW 607 zinatokana na gesi asilia, MW 566.7 unatokana na umeme wa nguvu ya maji na MW 183.9 ni mafuta na tungamotaka.

Dkt. Kalemani imeieleza Benki ya Dunia kuwa Serikali imekuwa ikisimamia utekelezaji wa TANESCO, ufuatiliaji wa madeni na malipo yanayohusu Shirika hilo na kudhamini TANESCO wakati wa uombaji wa mikopo kutoka kwenye taasisi za fedha. (Bank guarantee)
Aidha, kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO Mhandisi Felchesmi Mramba aliieleza Benki ya Dunia kuwa hivi sasa huduma zinazidi kuboreshwa kutokana na mahitaji ya umeme na kuongeza kuwa Watanzania waliofikiwa na huduma hiyo wameongezeka kutoka asilimia 36 hadi asilimia 40.

Mhandisi Mramba aliongeza kuwa, ongezeko hilo limechangiwa na uboreshaji na ukarabati wa miundombinu ya umeme , ujenzi wa mitambo ya gesi asilia, udhibiti wa wizi wa umeme na kuongeza kuwa bado Serikali inaendelea kuboresha huduma hiyo.

Dkt. Kalemani aliishukuru Benki ya Dunia  kwa niaba ya Serikali kwa mchango mkubwa inayotoa hususan upande wa nishati ya umeme na kuahidi kuwa, TANESCO itaendelea kuboresha huduma zake kwa wananchi na kueleza kuwa gharama za uzalishaji wa umeme zinaendelea kushuka zaidi ili kila Mtanzania aweze kufikiwa na huduma hiyo kwa wakati na kwa gharama nafuu.   

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...