Na Mwamvua Mwinyi,Pwani 

MKUU wa mkoa wa Pwani,mhandisi Evarist Ndikilo,amepokea madawati 200 kutoka kwa jeshi la nchi kavu kikosi cha Msangani,ambayo yatasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa madawati mkoani hapo .

Aidha sekretarieti ya mkoa imefanya jitihada za makusudi kuomba wadau mbalimbali kuchangia upatikanaji wa madawati ambapo imepata madawati 1,000.

Akikabidhiwa madawati hayo na brigadia general JM.Mwaseba pamoja na brigadia general AS.Bahati kwa niaba ya mkuu wa jeshi la nchi kavu Msangani,meja general James Mwakiborwa,mhandisi Ndikilo ,alilishukuru jeshi hilo kwa kuunga mkono sekta ya elimu.

Alieleza kuwa kabla ya agizo la Rais John Magufuli la kuondoa changamoto ya uhaba wa madawati katika shule za msingi na sekondari,katika mkoa huo kulikuwa na upungufu wa madawati 5,451 katika shule za sekondari.

Alisema upande wa shule za msingi upungufu wa madawati ulikuwa ni 43,507 lakini kwasasa wanashukuru tatizo hilo linaelekea kumalizika na kuwa historia.

Mhandisi Ndikilo alisema wilaya ya Mkuranga ,Rufiji na Mji wa Kibaha ndio zilizokuwa na mapungufu makubwa ya madawati lakini wakurugenzi wa halmshauri za wilaya hizo walijipanga kukabiliana na hali hiyo.

Hata hivyo alisema mchango huo utawezesha wanafunzi kuondokana na kero ya awali waliyokuwa wakiipata hali iliyokuwa ikisababisha kushindwa kusoma katika mazingira bora.

“Kwa niaba ya mkoa nawashukuru jeshi la nchi kavu ,mmeonyesha ni sehemu ya jamii ya mkoa,mfikishieni salamu zangu za dhani kwa meja general Mwakiborwa,tutaendelea kuwaenzi na tunawaombea muendelee kulinda amani ya nchi”alisema.

Alitaja mikakati iliyowekwa kufanikisha suala hilo,kuwa ni pamoja na wakurugenzi kuunda kamati mbalimbali za kufuatilia utengenezaji wa madawati,mbao na magogo yaliyokamatwa na askari wa maliasili vilielekezwa kutengeneza madawati.

Mhandisi Ndikilo alisema halmashauri zilitumia vyanzo vyao vya mapato,kutafuta wadau wa ndani na nje ya wilaya na mkoa,kuitisha harambee,kuhamasisha jamii na kukarabati madawati yaliyochakaa kidogo.

Awali katibu tawala wa mkoa huo,Zuberi Samataba alieleza miongoni mwa wadau waliojitokeza kuchangia zoezi hilo mkoani humo ni jeshi la nchi kavu na ubalozi wa China. Wengine ni kampuni ya goodwill Tanzania ltd ya Mkuranga,mamlaka ya bandari Tanzania ,taasisi mbalimbali binafsi na za umma,kampuni ya tigo.

Samataba alisema madawati zaidi ya 1,000 kutoka kwa wadau hao yatagawiwa katika shule mbalimbali kulingana na mahitaji. Alisema sekretriet ya mkoa inaendelea kuwasiliana na wadau wengine kuendelea kuunga mkono juhudi za kufanikisha upatikanaji wa madawati.

Brigadia general JM.Mwaseba ,alisema wakati mkoa ukiendelea na juhudi zake kufanikisha adhma hiyo jeshi hilo limejitolea kutoa madawati hayo ili kumuunga mkono rais Magufuli .

Alisema madawati hayo yametengenezwa katika kiwanda cha nyumbu chini ya brigadia jeneral AS.Bahati. Afisa elimu mkoani Pwani,Yusuph Kipengele alisema mkoa umeshakamilisha madawati ya shule za msingi na sekondari kwa asilimia 99.

Alisema mojawapo kati ya matokeo ya elimu bila malipo ni ongezeko la wanafunzi na hivyo kusababisha ongezeko la mahitaji ya miundombinu na samani ikiwemo madawati . Kipengele alieleza kuwa upande wa sekondari awali mkoa ulikuwa na mahitaji ya madawati 47,276 yaliyokuwepo 42,795 upungufu ulikuwa 4,481 sawa na asilimia 10.47.

Kipengele alisema shule za msingi mkoa ulikuwa na mahitaji ya madawati 92,586 yaliyokuwepo ni 61,318 upungufu ulikuwa ni madawati 31,268 sawa na asilimia 33.77.
Mkuu wa mkoa wa Pwani mhandisi Evarist Ndikilo, wa katikati ,ambapo kulia ni kamanda wa jeshi la nchi kavu kikosi cha Msangani Brigedia Jenerari Jairos Mwaseba na kushoto ni Brigedia Jenerari A .S.Bahati wakiwa  wameketi kwenye moja ya madawati ambayo jeshi hilo limechangia Mkoani Pwani.  
Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akipokea moja ya madawati kutoka kwa Kamanda wa jeshi la nchi kavu kikosi cha Msangani ,Brigadia Jeneral Jairos Mwaseba baada ya jeshi hilo kuchangia madawati 200 katika mkoa wa Pwani, Kulia ni Brigedia Jenerari A .S.Bahati (Picha na Mwamvua Mwinyi) 


Mkuu wa mkoa wa Pwani Mhandisi Evarist Ndikilo akimshukuru Kamanda wa jeshi la nchi kavu kikosi cha Msangani ,Brigadia Jeneral Jairos Mwaseba baada ya jeshi hilo kuchangia madawati 200 katika mkoa wa Pwani.
 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...