Na Editha Karlo wa blog ya jamii,Kagera.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya nchi Mhe. Mwigulu Nchemba amemtaka mkuu wa magereza mkoa wa Kagera(RPO) Kamishna Mwandamizi Jeremiah Nkonda kuwahamisha wafungwa walioko katika gereza la Kitengule la wilayani Karagwe na kuwapeleka gereza jirani la Mwisa kutokana na tetemeko la ardhi lililo tokea hivi karibuni mkoani hapa na kuharibu miundombinu na mabweni ya kulala wafungwa katika gereza hilo.

Waziri Nchemba alisema kauli hiyo baada ya kufanya ziara ya siku moja  Mkoani hapa na kutembelea taasisi zilizo chini ya wizara yake kwa lengo la kuona uharibifu uliojitokeza kutokana na tetemeko hilo .

"Nimetembelea magereza yetu lakini gereza la Kitengule limeharibika sana. Kuta zimeanguka mabweni yameharibika  kwa kiwango kikubwa kiasi kwamba hawapaswi kuishi watu. Kwa hiyo, naagiza mkuu wa magereza hapa kuwahamishia wafungwa hawa katika gereza la Mwisa lenye mabweni manne yaliyoko  wazi" alisema Nchemba.

Alisema ndani ya wiki moja zoezi hilo liwe limekamilika kwani wakiendelea kuwaacha wafungwa hao humo ni hatari kwani wanaweza kudondokewa na kuta zinazoning'inia na kusababisha kuwapoteza watu hao.

Alisema kutokana na tukio hilo Wizara inaandaa mpango wa Muda mrefu wa kujenga bweni kubwa litakalokuwa na uwezo wa kubeba wafungwa 400 kwa wakati mmoja kwani hilo ni gereza  la kikazi ambalo linabeba watu wengi.

Kamishna mwandamizi Jeremiah Nkonda alisema kilichochangia sana kushuka Kwa kuta hizo ni kwamba matofali yaliyojenga kuta hizo yanaonekana yalikuwa mabichi hivyo   haitowezekana kufanya ukarabati bali ni kubomoa mabweni hayo na kuyajenga upya.

Alisema gereza hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba wafungwa 380  Kati ya hao 100 wako Kwenye kambi ndogo ambapo 280 ndio watakaohamishiwa katika gereza la Mwisa.

  Waziri Mwigulu Nchema akipata maeleozo mafupi kuhusiana na ofisi ya Askari wa doria majini (Marine police) iliyobomoka kutokana na tetemeko la ardhi
 Waziri Mwigulu Nchema akikagua ofisi ya Askari wa doria majini(Marine police) iliyobomoka kutokana na tetemeko la ardhi
Waziri Mwigulu Nchemba akikagua makazi ya askari magereza wa Kitengule zilizobomoka kutokana na tetemeko la ardhi.  
 Waziri Mwigulu Nchemba akiangalia sehemu ya nyuma ya gereza la Kitengule ambalo ukuta wake umebomoka kutokana na tetemeko la ardhi.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Hahahahaha sehemu ya nyuma ya gereza ngoma bati na miti.....si muwaachie tu muanze na moja baada ya jengo jipya. Mnakomaa nao tu!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...