Na. Abushehe Nondo na Immaculate Makilika- MAELEZO

Jaji Mkuu wa Tanzania Mohamed Chande Othman amesema kuwa Serikali inatarajia kuzindua mpango mkakati wa Mahakama ya Tanzania kwa miaka 5 unaolenga kuboresha huduma za kimahakama nchini.

Aidha Jaji Mkuu alisema uzinduzi wa mpango huo utaenda sambamba na mradi wa maboresho wa huduma za utoaji haki nchini uliogharimu kiasi cha Tsh Bilioni 140.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam Jaji Chande alisema kuwa mradi huo una nguzo tatu ambazo ni utawala bora na uwajibikaji , fursa ya kutoa na kupata haki na uharakishaji wa mashahuri ambapo kwa pamoja umekusudia kutoa haki kwa wote na kwa wakati.

“Katika kujenga imani ya wananchi kwa mahakama tunataka kufikia sehemu ambapo mtu yeyote akileta shauri lake Mahakamani basi litasikilizwa kwa wakati” alisema Jaji Chande.

Aliongeza kuwa taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa asilimia 47 ya Watanzania hawana fursa sawa ya kupata haki ya Mahakama katika maeneo waliopo hususani mikoani kwa kuwa mikoa mingi haina Mahakama Kuu, hivyo mpango huo utakaozinduliwa utalenga kuboresha utendaji na utoaji huduma za kimahakama nchini.

Akizungumzia kuhusu mradi wa maboresho ya huduma za Mahakama ambao unaandaliwa kwa ushirikiano wa Serikali ya Tanzania na Benki ya Dunia Jaji Chande alisema kuwa mradi huo unalenga kuimarisha mifumo ndani ya Mahakama, kuendesha kesi na utoaji wa hukumu kwa wakati.

Jaji Chande aliongeza kuwa mradi huo utapanua wigo wa utoaji huduma za kimahakama ambapo itatoa fursa za mafunzo endelevu kwa watumishi wa Mahakama 6400 wa ngazi mbalimbali.

Aidha alisema mpango huo utasaidia kuimarisha Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kukijingea uwezo wa kutoa taaluma bora kwa watumishi pamoja na wadau katika masuala ya Sheria.

Jaji Chande alisema tayari mradi huo umewezesha kujengwa kwa Mahakama tano za kisasa zilizopo katika maeneo ya Kibaha, Kawe, Kisarawe, Kigamboni na Bagamoyo ambazo zitakuwa mfano wa uanzishwaji wa Mahakama za kisasa nchini.

Mradi huo unaogharimu bilioni 140 utazinduliwa Kibaha mkoani Pwani Septemba 21 mwaka huu, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...