Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amemaliza ziara yake ya siku NNE mkoani Mtwara kwa kuwahakikishia mamia ya wakazi wa wilaya ya Tandahimba mkoani Mtwara kuwa serikali imetenga zaidi ya bilioni 170 kwa ajili ya utekeleza wa mradi mkubwa wa maji katika wilaya hiyo ili kuondoa tatizo la uhaba wa maji kwa wananchi wa Tandahimba.

Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa kauli hiyo kwa nyakati tofauti wakati akihutubia mkutano wa hadhara mjini Tandahimba na wakati amesimamishwa njiani na wananchi wa vijiji vya Kitama I na Kitama II ambao walitaka kumsalimia akiwa katika ziara yake ya kikazi wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.

Makamu wa Rais amesema mkakati wa serikali wa sasa unalenga kuhakikisha wananchi wa Tandahimba na wa maeneo mengine nchini wanapata maji safi na salama hali ambayo itaondoa usumbufu wa wananchi kutumia muda mwingi kutafuta maji badala ya kufanya shughuli za maendeleo.

Amesema anaimani kubwa kuwa mradi huo wa maji utakapokamilika wilayani Tandahimba mkoani Mtwara utakuwa ni suluhu ya kudumu ya uhaba wa maji kwa wananchi hao wa Tandahimba.

Kuhusu usafirishaji wa korosho kwa njia ya magendo, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameonya kuwa serikali kamwe haiwezi kuwavulia watu wanaofanya vitendo hivyo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali za kisheria ili kukomesha tabia hiyo.

Makamu wa Rais amesema kuwa biashara ya magendo ya korosho inainyima serikali mapato mengi ambayo yangesaidia shughuli za maendeleo za wananchi hivyo ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mtwara uchukue hatua za kukomesha biashara hiyo haramu ambavyo ameifananisha na uhujumu uchumi kwa serikali.

Kuhusu ubovu wa barabara kutoka mjini Mtwara hadi wilaya ya Tandahimba, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amesema serikali itajenga kilomita 50 za awali kwa kiwango cha lami katika barabara hiyo ili kuimarisha shughuli za usafiri na usafirishaji kati ya Mtwara mjini na wilaya ya Tandahimba.

Makamu wa Rais pia ameuagiza uongozi wa mkoa wa Mtwara kukutana haraka na Watendaji wa Wakala wa Barabara wa mkoa wa Mtwara ili kujadiliana kuhusu namna gani ujenzi huo utakavyotekelezwa.

Akiwa mjini Tandahimba, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika zoezi la utoaji wa zawadi mbalimbali kwa uongozi wa shule ya sekondari ya Tandahimba kwa kuingia katika shule 10 bora kitaifa katika matokeo ya Kidato cha Sita ambapo Kampuni ya Startimes imetoa hundi ya shilingi milioni Mbili kwajili ya ujenzi wa mabweni ya wanafunzi wilayani humo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akiwasalimia wakazi wa kijiji cha Kitema I wilayani Tandahimba  waliojitokeza kwa wingi kumlaki wakati akiwasili kwenye wilaya hiyo ikiwa sehemu ya ziara yake mkoani Mtwara.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokelewa kwa burudani ya ngoma wakati akiwasili kwenye makao makuu ya wilaya ya Tandahimba, mkoani Mtwara.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akihutubia wakazi wa wilaya ya Tandahimba  kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa Kiwanda cha kubangua korosho cha AMAMA kilichopo wilayani Tandahimba mkoani Mtwara.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipata maelezo kutoka kwa Msimamizi na Mdhibiti wa ubora wa bidhaa Bw. Karim Hassan (kushoto) ya hatua mbali mbali ambazo korosho hupitia wakati wa kubanguliwa kwenye kiwanda cha AMAMA kilichopo Tandahimba mkoani Mtwara.

BOFYA HAPA KWA PICHA ZAIDI

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...