Tanzania imekubali kuyatekeleza mapendekezo 131, kuyakataa
94, kuyakubali kiasi mawili kati ya mapendekezo 227 yaliyotolewa na mataifa
wanachama wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa. Taarifa ya
Serikali iliwasilishwa mbele ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa
na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Katiba na Sheria Profesa Sifuni Mchome (pichani) lililokaa
September 21 hadi 23, 2016.
Aidha, Baraza hilo limepitisha Taarifa hiyo ya pili ya
Tanzania ya Haki za Binadamu chini ya Mfumo wa Mapitio wa Umoja wa Mataifa kwa
Kipindi Maalum (Universal Periodic Review (UPR) Mechanism) katika kikao
kilichofanyika mjini Geneva nchini Uswisi.
Mapendekezo ambayo Tanzania imeyakubali yanahusu;
ukamilishaji wa Mchakato wa Katiba, kuijengea uwezo wa kifedha Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora, kutekeleza Malengo endelevu ya Dunia, Uandaaji wa
Taarifa za Nchi za Utekelezaji wa Masuala ya Haki za Binadamu, Utekelezaji wa Mpango
Kazi wa Haki za Binadamu, haki za wanawake na watoto, watu wenye ulemavu,
wazee, haki ya elimu, afya, maji, mazingira na mengineyo.
Aidha, Mapendekezo mawili
ambayo yalikubaliwa nusu yalikuwa na baadhi ya mambo ambayo yanaendana
na Katiba, Sera na Sheria za nchi na mambo mengine ambayo yanakinzana na hayo.
Masuala hayo yanahusu Serikali kuziwezesha Asasi za Kiraia kimuundo na kifedha
na kutoa fidia kwa wahanga wanaotokana na mashambulizi yanayofanywa kwa watu
wenye ualbino.
Mapendekezo ambayo Tanzania imeyakataa yanahusu suala la
hali ya kisiasa Zanzibar, Sheria ya Makosa ya Mtandaoni, uhuru wa kupata
taarifa , adhabu ya kifo, utoaji mimba, mapenzi na ndoa za jinsia moja, ubakaji
ndani ya ndoa na umiliki wa ardhi kwa kuwa yanakwenda kinyume na Katiba, Sheria,
Sera, Dini na Tamaduni za nchi kwa ujumla.
Akiwasilisha taarifa hiyo ya Serikali, Prof Mchome amesema
Serikali imejidhatiti kutekeleza mapendekezo yote yaliyokubaliwa na kuongeza
kuwa Tanzania inaunga mkono Azimio la Vienna na kwamba itaendelea kutekeleza
mpango wa Taifa wa Haki za Binadamu.
“Tumejidhatiti kutekeleza mapendekezo tuliyoyakubali na
tutaendelea kuimarisha taasisi ya Taifa ya Haki za Binadamu kwa kuipatia
rasilimali fedha, watu na vifaa ili ifanye kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo
kwa mtindo wa haki za binadamu,” alisema.
Pia alisema kuwa kuna baadhi ya mapendekezo ambayo Serikali
imeyachukua kwa ajili ya kuyafanyia kazi. Mapendekezo hayo ni pamoja na haki za
watu wenye ualbino, adhabu ya viboko na haki ya mtoto kuandikishwa bure baada
ya kuzaliwa ili apatiwe cheti cha kuzaliwa.
Profesa Mchome alisema Serikali imepokea mapendekezo matatu
kuhusu haki za watu wenye ualbino ambayo yanataka Serikali kuifanyia mabadiliko
Sheria ya Dawa na Tiba Mbadala ya mwaka 2002 ili kuwazuia waganga kutowadhuru
watu wenye ualbino na kuahidi kuwa wataipitia upya.
Alisema kuwa Serikali imepokea na kukubali sehemu ya pendekezo la kuzisaidia kifedha na kimuundo asasi
zinazojishughulisha na masuala ya watu wenye ualbino. “Tumepokea na kukubali
sehemu ya pendekezo hilo ambalo linaitaka Serikali kuzisaidia kifedha na
kimuundo asasi zinazojishughulisha na masuala ya watu wenye ualbino,” alisema.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...