Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jumhuri William akipiga mpira katika eneo la penati kuashiria kuwa mashindano ya Mgimwa Cup yamezinduliwa rasmi.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jumhuri William aliyeshika mpira kulia sambamba na Mwenyekiti wa CCM Mufindi, Yohanis Kaguo aliyeshika mpira kushoto wakiwa na baadhi ya wachezaji
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jumhuri William akikagua timu kabla mtanange kuanza.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jumhuri William akikagua timu kabla mtanange kuanza huku akiwapa neno wachezaji wa timu husika katika kiwanja cha Ikwea.

Na Fredy Mgunda, Iringa. 

MASHINDANO ya kombe Mgimwa Cup yamezinduliwa rasmi katika kijiji cha Ikwea kata ya Ikwea wilayani Mufindi mkoani Iringa kwa kushirikisha timu za vijiji vyote vya jimbo la Mufindi Kaskazini kwa lengo la kuinua vipaji kwa wachezaji wa jimbo hilo.

Akizindua mashindano hayo yaliyofanyika Kiwanja cha Ikwea katika kijiji cha Ikwea Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Jumhuri William kwa niaba ya Mbunge wa Jimbo la Mufindi Kaskazini alisema ni wakati mzuri kwa sasa kuyageukia mashindano ya mchangani kwani yamesheheni vipaji vingi vitakavyosaidia kuendeleza mpira wa Tanzania wakati ambapo Taifa likiendelea kupata matokeo yasiyoridhishwa kwenye soka kwa sasa.

"Mashindano haya ni muhimu sana kwa wakati huu kwani yatasaidia kuinua vipaji vya vijana wetu na kuweza kupata timu bora ya taifa, hivyo nidhamu ni muhimu wakati wa michezo hiyo" alisema William

Aidha Wiliamu aliongeza kwa kusema kuwa mpira wa miguu umekuwa na faida kwa wachezaji kwani wanaweza kujitengezea vyanzo vya ajira kama Mbwana Samatta na wachezaji wengine wakulipwa hapa nchini hata nje ya nchi.

“ Soka limewapa ajira mamilioni ya wachezaji na viongozi ulimwenguni na wameweza kuishi maisha ya kifahari kutokana na mishahara wanayopata”, alisema William.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano hayo Felix Nyimbo aliwataka washiriki wa mashindano hayo kujituma ili ipatikane timu ya kata ambayo itakuwa ikiwakilisha kata hiyo katika mashindano ya wilaya, kanda hadi taifa.

Kwa upande wake mlezi wa Mashindano hayo Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wilaya Mufindi, Yohanes Kaguo alisema ataendelea kuwaunganisha vijana kupitia michezo na kusaidia kukuza michezo wilaya ya Mufindi.

Mashindano ya Mgimwa Cup ni miongoni mwa mashindano yanayolenga kuibua vipaji vya vijana vijijini ili kuwawezesha kupata nafasi ya kucheza katika vilabu vikubwa nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...