NCHI za Afrika wanachama wa Shirikisho la Riadha la Kimataifa (IAAF), zimetakiwa kuendesha kozi mbalimbali ili kuibua wataalamu wengi wa mchezo huo katika ngazi za kimataifa.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Kituo cha Maendeleo cha Kikanda cha IAAF-Nairobi, Kenya, Ibrahim Hussein, wakati wa ufungaji wa Semina ya Masoko kwa Michezo (IAAF Sports Marketing), iliyofanyika jijini humo hivi karibuni.

Ibrahim, alisema kumekuwa na uhaba mkubwa wa wataalamu mbalimbali katika mchezo wa riadha kimataifa kama Olimpiki, Mashindano ya Dunia nk. Jambo ambalo halipendezi, hivyo mashirikisho ya Riadha ya Nchi za Afrika yanapaswa kuwaandaa watu wao na Kituo chake kiko tayari kuwaendeleza katika ngazi za kimataifa.

“IAAF imekuwa ikiendesha kozi mbalimbali kama za ukocha, uamuzi, ufundishaji wa watoto na safari hii kozi ya ‘Marketing’, hivyo nendeni mkafundishe watu wenu na mimi niko tayari kuandaa mtandao na kisha kuwaendeleza katika ngazi za kimataifa,” alisema Ibrahim.

Mkurugenzi huyo, alibainisha kuwa kozi za awali ‘Level I’ ni kazi ya mashirikisho ya nchi na kuendelea ngazi ya pili ‘Level II’ na ya tatu ‘Level ‘III’ ni ya IAAF na yeye kama mkurugenzi wa Kanda ya Nairobi, yuko tayari kufanikisha katika hilo ili kuwezesha waafrika wengi zaidi kushiriki katika matukio ya riadha ya kimataifa.

Akiwazungumzia washiriki wa kozi hiyo ya masoko katika michezo, aliwataka kwenda kuyatumia vema mafunzo waliyoyapata kwa manufaa ya nchi zao na kwamba, watambue kuanzia sasa si mali ya mashirikisho ya nchi zao bali IAAF na wawe tayari kutumika sehemu yoyote watakapotakiwa.

Kwa upande wake Mkufunzi wa semina hiyo, Dk.Christoph Bertling kutoka Kitengo cha Mawasiliano na Utafiti wa Vyombo vya Habari (Instute of Communication and Media Research), Chuo Kikuu cha Michezo cha Cologne Ujerumani (German Sport University Cologne), alielezea kufurahishwa na ushirikiano ulioonyeshwa na washiriki wa semina hiyo na kuwataka kutokwenda kujifungia na ujuzi waliopata, bali wautumie kwa manufaa ya maendeleo ya mchezo wa riadha nchini mwao.

Dk. Bertling, aliwasihi washiriki hao kutosita kuendelea kuwasiliana naye kwa ushauri na kwamba hatosita kutoa msaada pale atakapoombwa.
Semina hiyo iliyofanyika hoteli ya Kasarani Sport View, ilishirikisha washiriki kutoka nchi 16 zinazozungumza lugha ya Kiingereza.

Washiriki hao ni pamoja na Stephen O. Bamiduro, Almu Umar Lambu (Nigeria), Cortex Nzima (Malawi), Phineas Mukwazo (Zimbabwe), Dk. Marc Dzradozi (Ghana), Sejanamane Maphathe (Lesotho), Bisrat A. Sileshi (Ethiopia), na Apollo B.Musherure (Uganda).

Wengine ni Tullo Stephen Chambo (Tanzania), Dennis Skrywer (Namibia), Bernard T. Kajuga, Patrick Thierry (Mauritius), Esayas Ande (Eritrea), Susan Kamau, Evans Bosire, Joseph Kipchumba, Karen Gachahi na Sally Rama (Kenya).

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...