Kampuni ya uchimbaji wa gesi ya PanAfrican Energy Tanzania imekabidhi msaada wa mabati 1900 na mifuko 5000 saruji kwa wahanga wa tetemeko la ardhi Kagera. Msaada huo uliokabidhiwa kwa Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu ofisini kwake ni kutoa mkono wa pole kwa wana Kagera kwa maafa yaliyowakumba takribani siku kumi zilizopita. 

Akikabidhi msaada huo Meneja Uwajibikaji kwa jamii wa Kampuni ya PanAfriacan Energy Tanzania Limited Bwana Andrew Kashangaki alisema, “Kwa niaba ya Kampuni ya PanAfrican Energy tunatoa pole kwa watanzania wenzetu wana Kagera kutokana na janga lililowakumba ndugu zetu na kuwahakikishia tupo pamoja katika hili.Kwa uzalendo mkubwa tumeguswa na yaliyowapata wenzetu na hasa kupata uharibifu mkubwa wa mali na mbaya zaidi kupoteza uhai wa baadhi ya watanzania wenzetu pia kupata majeruhi. 

Hili ni janga letu sote kwa kuguswa na hili tumekabidhi mifuko 5000 ya saruji na mabati 1900 ambayo tunaamini yatasaidia kufanyia marekebisho baadhi za nyumba zilizoathiriwa na tetemeko. Kwa hiki kidogo tunaomba kiwe kama faraja kwenu na tunawahakikishia hatutaishia hapa tutaendelea kusaidia kadiri ya mahitaji ya wenzetu hasa katika elimu yaani kufanyia ukarabati baadhi za shule zilizoharibika vibaya. 

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya PanAfrican Energy Patrick Rutabanzibwa aliushukuru uongozi wa mkoa wa kagera kwa namna wanavyozidi kujaribu kutatua changamoto wanazopitia waathirika wa tetemeko ardhi. Alielezea namna wanavyojitokeza kusaidia shughuli za kijamii, “Kampuni yetu inashughulika na utafutaji, uchimbaji, uendelezajii na usambazaji wa gesi asili ya Songo Songo.

Kampuni ilianza shughuli hizi mnamo Mwaka 2001 na uzalishaji ukaanza 2004. PanAfrican Energy (Tanzania) inafanya miradi ya maendeleo ya kiuchumi, kisheria na kimaadili, katika kutatua matatizo ya jamii zetu na kujitolea uwezo wetu, rasilimali na watu katika kujenga maisha bora ya baadaye kwa wote. Miradi ya PanAfrican Energy (Tanzania) itatathiminiwa na kukubaliwa katika misingi ya kudumu kwenye sekta ya elimu, afya na uwezeshwaji wa jamii. 

Tunaamini huu ni mwanzo wa kushirikiana na wewe. Tumeweza kutembelea sehemu mbali mbali na kuona shule zilizopata uharibifu mkubwa na tunaahidi kwamba tukirudi Dar es Salaam tutawasilisha ujumbe huu na kwamba bado msaada unahitajika kurudisha shule zetu kwenye hali ya kawaida.” 

Akipokea msaada huo Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu aliishukuru Kampuni ya PanAfrican Energy kwa msaada wa vifaa vya ujenzi waliowapatia na kutoa wito kwa wadau wengine kuendelea kusaidia. 

“Hii inadhihirisha ni jinsi gani watanzania tulivyo na umoja na upendo, kwa niaba ya wana Kagera na Serikali kwa ujumla natoa shukrani zangu za dhati kabisa kwa msaada huu mkubwa militupatia wa vifaa vya ujenzi. Bado tunahitaji msaada zaidi kwani athari iliyotokea ni kubwa sana kuachilia vifo vya wenzetu 17 bado majengo mengi yameathirika vibaya kwani majengo 2072 yamebomoka kabisa, zaidi ya 40,000 yapo katika uharibifu hatarishi na 9000 yana mipasuko”. 

Msaada huo ulitolewa mara baada ya mkoa wa Kagera kupatwa na tetemeko la ardhi lililotokea takribani siku kumi zilizopita.

Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu akimshukuru Meneja Uwajibikaji kwa jamii wa Kampuni ya PanAfriacan Energy Tanzania Limited Bwana Andrew baada ya kukabidhiwa msaada wa mabati 1900 na mifuko 5000 yasaruji kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera
Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu akizungumza jambo na uongozi wa kampuni ya PanAfriacan Energy Tanzania Limited baada ya kukabidhiwa msaada wa mabati 1900 na mifuko 5000 yasaruji kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera
Mkuu wa mkoa wa Kagera Meja Jenerali mstaafu Salum Mustafa Kijuu akimshukuru Patrick Rutabanzibwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya kampuni ya Pan African Energy baada ya kukabidhiwa msaada wa mabati 1900 na mifuko 5000 yasaruji kwa waathiriwa wa tetemeko la ardhi mkoani Kagera.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...