Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amezindua kivuko kipya na cha kisasa cha Mv. Tanga kinachotoa huduma ya usafirishaji kati ya Pangani na Bweni na kuzindua Gati ya Bandari ya Pangani wilayani pangani mkoani Tanga.

Akizungumza katika uzinduzi huo Waziri Mbarawa amesema kuwa ujio wa kivuko hicho utafungua fursa za kibiashara na kuchochea maendeleo ya kiuchumi wilayani hapo. “Naamini ujio wa kivuko hiki utarahisisha huduma za kijamii na maendeleo ya kiuchumi wilayani hapa, hivyo naomba mkitunze vizuri kivuko hiki ili kiweze kudumu kwa muda mrefu”, amesema Prof.Mbarawa.50 242

Ameongeza kuwa katika kuhakikisha huduma za kivuko zinakuwepo muda wote wilayani hapo, Serikali kupitia Wizara hiyo imetenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa boti ambayo itatumika kama mbadala wa usafiri wakati wa usiku katika maeneo hayo ambapo kivuko cha Mv.Tanga hakifanyi kazi.

Kuhusu ujenzi wa Gati ya bandari ya Pangani Waziri Mbarawa ameseama kuwa ujenzi wa gati hiyo utapelekea Meli kubwa kuweza kutia nanga na kurahisisha usafiri wa moja kwa moja kutoka Pangani kwenda visiwa vya Unguja na Pemba. Amefafanua kuwa Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wataanzisha huduma ya boti za haraka kutoka Pangani kwenda Mkokotoni Zanzibar hivyo kufungua fursa za kibiashara na kitalii baina ya Tanga na Zanzibar.

Kwa upande wa huduma za mawasiliano ya simu wilayani hapo, Prof.Mbarawa amesema kuwa huduma hiyo itaanza mwezi Desemba mwaka huu kwa mkandarasi kufika na kuanza ujenzi wa miundombinu ya simu na hivyo kuondoa tatizo la mawasiliano wilayani hapo.

Katika hatua nyingine Prof. Mbarawa amehahidi kuanza ujenzi wa Barabara ya Tanga-Pangani-Saadani hadi Bagamoyo (KM 242) kwa kiwango cha lami ifikapo mwakani. Amefafanua kuwa ujenzi wa barabara hiyo utakuwa wa awamu ili kuweza kuharakisha kukamilika kwake ambapo awamu ya kwanza itahusisha kipande cha barabara ya Tanga- Pangani (KM 50) na kuongeza kuwa ujenzi wa barabara hiyo utafungua fursa za kiuchumi kati ya Tanga na Pangani.

“Naahidi kujenga barabara hii ambayo ni kiungo kati ya Tanga na Pangani, naamini ukamilifu wake utalete maendeleo mkoani hapa”. Amesisitiza Prof. Mbarawa. Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Eng.Joseph Nyamhanga amezipongeza kampuni za Songoro Marine na Alpha Logistic kwa kumaliza kwa wakati ujenzi wa kivuko na Gati ya bandari hiyo.

Naye Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA) Eng.Manase Ole-kujan amesema kuwa kivuko cha Mv.Tanga kimejengwa kwa sh.bilioni nne ambapo kina uwezo wa kubeba tani 50 abiria 100 na magari madogo 6 kwa wakati mmoja.

Ujenzi wa Kivuko cha Mv. Tanga ni moja ya utekelezaji wa ahadi ya Mhe.Rais Dkt.John Pombe Magufuli aliyoitoa wakati wa kampeni ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 wilayani Pangani Mkoani Tanga.

Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na watendaji wa Serikali na Wizara wakikata utepe kuashiria uzinduzi rasmi wa Kivuko cha Mv. Tanga kulia ni Mkuu wa wilaya ya Pamgani Mhe. Zainabu Abdallah Issa . 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa pamoja na watendaji wa Serikali na Wizara wakizindua Gati la Bandari ya Tanga.Ukamilifu wa Gati hiyo utasaidia Meli mbalimbali kuweza kutia nanga wilayani Pangani. 
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (wa pili kulia) akisafiri na wakazi katika Kivuko cha Mv.Tanga kutoka Pangani kwenda Bweni mara baada ya uzinduzi. Wanne kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo (Sekta ya Ujenzi) Eng. Joseph Nyamhanga.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...