Naibu Katibu Mkuu wa Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo (wa pili kutoka kulia waliokaa mbele) akisikiliza mada iliyokuwa ikitolewa na Balozi Mkazi wa Norway nchini, Hanne-Marie Kaarstad (hayupo pichani) katika Semina iliyofanyika jijini Dar es Salaam, iliyolenga kukutanisha Wadau mbalimbali wa Nishati ya Umeme na Taasisi za nishati ya umeme Nchini Norway.
Kaimu Kamishna wa Nishati anayeshughulikia Umeme, Mhandisi Innocent Luoga (wa pili kutoka kulia) akielezea Sera za Nishati za Umeme za Tanzania kwa wadau mbalimbali walioshiriki Semina hiyo. Wengine katika picha ni Viongozi Waandamizi kutoka Taasisi za Wizara ya Nishati na Madini.

Na Rhoda James.
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Nishati, Dkt. Mhandisi Juliana Pallangyo amesema kuwa, Serikali ya Tanzania imefanya mageuzi makubwa katika Sekta ya Nishati ya Umeme ikiwa ni moja ya mikakati ya kupunguza umaskini kwa wananchi wa Tanzania.

Dkt. Pallangyo aliyasema hayo hivi karibuni katika Semina iliyofanyika katika Hotel ya Serena jijini Dar es Salaam, lengo likiwa ni kukutanisha Taasisi za Norway na Wadau wa Nishati ya Umeme nchini.

Akifungua Semina hiyo, Dkt. Pallangyo alisema kuwa, Semina hiyo ni fursa kwa Wadau wa Nishati ya Umeme kujifunza na kubadilishana uzoefu kwa kuwa nchi ya Norway ni miongoni mwa nchi kubwa Duniani ambayo inazalisha nishati ya umeme kwa kutumia nguvu ya maji, gesi na mafuta.
“Serikali ya Norway ina uzoefu mkubwa katika Sekta ya nishati ya umeme inayozalishwa kwa nguvu ya maji kwa kuwa hadi sasa nchi hiyo inazalisha nishati hiyo kwa kutumia nguvu ya maji kwa asilimia 95,” alisema Dkt. Pallangyo. 

Aidha, Dkt. Pallangyo kwa niaba ya Serikali ya Tanzania aliishukuru Serikali ya Norway kwa ushirikiano inaotoa kwa Tanzania hususan katika Sekta ya Nishati huku akielezea kuwa, ushiriki wa Taasisi binafsi katika kuzalisha nishati hiyo ni muhimu kwa kuwa Serikali yenyewe haiwezi kufanya kila kitu.

Kwa upande wake, Balozi Mkazi wa Norway Nchini, Hanne-Marie Kaarstad alieleza kuwa, ushirikiano wa nchi hizo mbili ni wa muda mrefu kutoka miaka ya 1900 na kwamba ushirikiano huo ni wa kipekee.

Balozi Kaarstad alisema kuwa, katika Semina hiyo kampuni zaidi ya 80 na Wadau mbalimbali nchini walishiriki mkutano huo huku Kampuni 14 za Norway zilizoshiriki.

Alisema kuwa, Taasisi binafsi ni wadau muhimu katika sekta ya nishati, hii ni fursa muhimu kwa wadau mbalimbali nchini kujifunza kutoka kwa Taasisi za Norway kwa kuwa wanao uzoefu mkubwa katika sekta hii.

Taasisi zilizoshiriki katika semina hiyo ni pamoja na Kampuni ya Norwegian Investment Fund for Developing Countries (NORFUND), Jacobsen Elektro, Statoil’s Renewable Energy, Rift Valley Energy, Viking Heat Engines na Rainpower Norway. Nyingine ni Bergen Engines, Multiconsult, W. Giertsen Energy, Eltek, Standard Hydro Power, Norsk Vind Energi, Green Resources, SN power na The International Centre for Hydropower

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...