Na: Lilian Lundo - MAELEZO

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imejizatiti kuondoa tabaka la wasiojua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa vijana na watu wazima kwa kujenga uwiano sawa wa utoaji wa elimu kwa watu wote.

Hayo yamesemwa na Kaimu Kamishna wa Elimu kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Bw. Nicholaus Bureta ambaye alimuwakilisha Mgeni Rasmi, Katibu Mkuu wa wizara hiyo katika Maadhimisho ya Siku ya Kisomo Duniani, yaliyofanyika leo, katika viwanja vya Makumbusho ya Taifa Jijini Dar es Salaam.

“Wizara imejipanga vizuri, na lengo kubwa la wizara ni kuhakikisha tunakuwa na mtanzania aliye elimika na aliye na stadi, maarifa na uwezo wa kutumia elimu aliyoipata,” alifafanua Bureta.

Vile vile Bw. Bureta amesema kwa sasa wizara ipo kwenye mpango wa kukuza stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) ambao unaanzia chini kwa wanafunzi wa awali mpaka shule za msingi.

Katika mpango huo walimu wamekuwa wakipata mafunzo mbalimbali ya namna ya kumuwezesha mwanafunzi kujua Kusoma Kuandika na Kuhesabu katika ngazi ya elimu ya awali.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Msaidizi Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, Basilina Levira amesema kwamba kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012, asilimia 78 ya vijana na watu wazima ndio waliokuwa wakijua kusoma na kuandika.

Akaongeza kuwa mwaka 2015 idadi hiyo ya wanaojua kusoma na kuandika ilishuka na kufikia asilimia 77 ambapo ilipelekea wizara hiyo kutoka na mikakati inayokusudia kuondoa kabisa tabaka la watu wasiojua kusoma na kuandika nchini.

Aidha, Basilina amesema kuwa Serikali ilipitisha sheria ya vyumba vya madarasa ya shule zote nchini kutumika kufundishia vijana na watu wazima ambao hawajui kusoma na kuandika muda wa jioni baada ya wanafunzi wa kawaida wanapomaliza masomo yao.

Amefafanua kwa kusema kuwa, wizara imeandaa programu ambayo iko kwenye mfumo wa Televisheni na picha za video (DVD) yenye masomo 65 ya kujifunza kusoma, kuandika na kuhesabu, ambapo kwa kutumia program hiyo mwanafunzi anaweza kujua kusoma, kuandika na kuhesabu kwa muda wa miezi 4 mpaka 6.

Mafunzo hayo kwa njia ya Televisheni na Picha za Video tayari yameanza kutumika kwa wilaya za Ilemela, Dodoma Manispaa, Songea Manispaa, Bagamoyo, Mkuranga, Temeke, Ilala na Kinondoni, ambapo asilimia 65 ya vijana na watu wazima wasiojua kusoma na kuandika wamejitokeza kujiunga na Elimu hiyo huku idadi kubwa ikiwa ni ya wanawake.

Siku ya Kisomo Duniani huadhimishwa Duniani kote kila ifikapo Septemba 08 ya kila ya mwaka, ambapo mwaka huu 2016 maadhimisho hayo yametimiza miaka 50 tangu yalipoanza kuadhimishwa mwaka 1966.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...