Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu
Na Eleuteri Mangi, MAELEZO, Bukoba.

Serikali imesema gharama za kujenga upya shule za sekondari za Ihungo na Nyakato ni Sh. Bilioni 60 hadi kukamilika miundombinu yake ambayo itakayoruhusu wanafunzi kupata elimu kama kawaida. 
Hayo yamesemwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Meja Jenerali Mstaafu Salum Kijuu leo mjini Bukoba alipokuwa akitoa taarifa kwa waandishi wa habari kuhusu hatua zilizochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na athari zilizosababishwa na tetemeko la ardhi lililoukumba mkoa huo. 
Katika kukamilisha ujenzi wa shule hizo, Mkuu wa mkoa amesema kuwa hatua ya kuvunja majengo yote imeshaanza ambapo tayari Kampuni ya CHICO ya Wachina inaendelea na uvunjaji wa majengo yote ili kazi ya ujenzi uanze.. 
“Wataalam wote wa ujenzi kutoka idara mbalimbali za Serikali wanaendelea na uchambuzi yakinifu wa majengo mapya ya shule hizo utakaozingatia viwango vya ujenzi ambapo ghrama za awali kwa tathmini iliyotolewa na wataalamu hao ni Sh. bilioni 30 kwa shule za Ihungo na Nyakato” alisema Meja Jenerali Mstaafu Kijuu.

Uamuzi wa kuzijenga shule hizo upya zilizoharibiwa na tetemeko la ardhi, ulipelekea Serikali kuzifunga na kuwahamisha wanafunzi waliokuwa wanasomea katika shule za Sekondari Ihungo na Nyakato ili waweze kuendelea na masomo wakati shule zao zinajengwa upya. 
Wanafunzi wa shule hizo tayari wamepangiwa shule watakazoenda ili kuendelea na masomo kulinhgana na mihula ya mwaka na ratiba za vipindi vya masomo kila siku. 
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesma kuwa katika kuhakikisha ujenzi wa majengo ya taasisi za Serikali na wananchi yanakuwa imara na salama, wataalam wa Wakala wa Jiolojia Tanzania ndio watatoa ushauri wao kabla ya ujenzi mpya haujaanza ili ujenzi wa majengo mapya ufanyike sehemu sahihi. 
Kuhusu misaada inayotolewa na Serikali, nchi rafiki, wadau na wananchi, Mkuu wa Mkoa amesema kuwa Kamati ya Maafa katika kukabiliana na athari za tetemeko kwa wananchi walioathirika tayari imetoa mahitaji mbalimbali kwa waathirika wa tetemeko hilo. 
Mahitaji yaliyotolewa kwa wananchi ni pamoja na unga wa sembe kilo 3,450, sukari mifuko 410, mchele kilo 3,150, maharage kilo 5,753, maji katoni 850, sabuni katoni 24, mashuka 90, mablanketi ya watu wazima na watoto 2,020, vyandarua 1,274, sare za wananfunzi 570, magodoro 694, mahema 127 na matrubali 2,760. 
Aidha, mkuu huyo wa mkoa amezitaka Kamati za Maafa za Wilaya zikarabati miundombinu ya kutolea huduma za kijamii ikiwemo shule za sekondari na msingi, vituo vya kutolea huduma za afya vilivyoharibiwa na tetemeko la ardhi ili huduma hizo muhimu ziweze kurejea mara moja na kutoa huduma kwa wananchi.
Hadi sasa wamebaki jumla ya majeruhi 13 ambapo katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wamebakia majeruhi tisa, Hospitali ya Mugana majeruhi wawili na Hospitali ya Rufaa ya Bugando majeruhi wawili ambao wanaendelea kupata huduma za matibabu na hali zao zinaendelea vizuri. 
Tetemeko la ardhi lililotokea Septemba 10, 2016 Mkoani Kagera lilisababisha vifo vya watu 17, majeruhi 440, majeruhi 427 tayari wametibiwa na kuruhusiwa katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa na vituo mbalibali vya afya kwenye mkoa.


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...