Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyekundu) akizungumza na wananchi wa Kata ya Mahembe, wilaya ya Kigoma Vijijini ambapo mradi wa Nishati Vijijini unatekelezwa.
 Baadhi ya wananchi wakimsikiliza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.
 Eneo ambalo miundombinu ya umeme imeathirika kutokana na uchomaji wa misitu. 

SHIRIKA la Umeme Tanzania (Tanesco) limeagizwa kufikisha elimu kwa wananchi kuhusu utekelezaji wa Miradi ya Umeme Vijijini na utunzaji wa mindombinu yake ili kuwaongezea uelewa na pia kuwahamasisha kuunganishwa na huduma hiyo.

Agizo hilo limetolewa jana Mkoani Kigoma na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati wa ziara ya kukagua Mradi wa Umeme Vijijini unaotekelezwa mkoani humo na Kampuni ya kitanzania ya State Grid.

Awali katika taarifa ya utekelezaji wa mradi husika kwa mkoa huo iliyowasilishwa na Mkandarasi kupitia Mkurugenzi wa kampuni, Wilbroad Mutabuzi ilielezwa kuwa hadi hivi sasa wananchi waliounganishiwa umeme mkoani humo ni 6,700 wakati lengo ni kuwaunganisha wateja 12,753.

“Wananchi wengi hawajajitokeza kuunganishiwa huduma ya umeme; mfano baadhi ya vijiji unakuta transfoma moja ina wateja 6 nyingine mteja mmoja jambo ambalo linaleta shida katika usambazaji,” ilielielezwa katika taarifa hiyo.

Mbali na hilo, Mkandarasi huyo alieleza kuhusiana na uchomaji hovyo wa misitu jambo ambalo alisema kwa mkoa mzima wa Kigoma limesababisha kiasi cha nguzo 27 kuungua  na kusababisha hasara za kusimika nguzo zingine na kubadili baadhi ya miundombinu.

Kufuatia taarifa hiyo pamoja na maswali yaliyokuwa yakiulizwa na wananchi wa maeneo ya mradi, ilibainika kuwa wananchi walio wengi hawana uelewa mzuri kuhusiana na mradi huo.

Profesa Muhongo alisisitia kuwa elimu ya mara kwa mara iendelee kutolewa ikiwemo kuelezea madhara watakayopata endapo nguzo zitaungua na moto.

Vilevile Profesa Muhongo alisema elimu ya nishati ya umeme kwa wananchi  itawawezesha kuufahamu mradi kwa kina, kuelewa umuhimu wake na kufahamu matumizi endelevu ya nishati ya umeme kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

Alisema kupitia elimu husika, wananchi watahamasika kujitokeza kwa wingi ili kuunganishiwa huduma hiyo hasa ikizingatiwa kuwa gharama za kuunganishwa ni shilingi 27,000 ambayo wengi wao wanamudu.

Aidha, Profesa Muhongo aliagiza ratiba ya utoaji elimu iandaliwe kwa ajili ya maeneo yote ya mradi na wakati huo huo aliwaasa wananchi kujitokeza kwa wingi ili kunufaika nayo.

Mbali na hilo, Waziri Muhongo aliwaasa wananchi hao kuepuka kutumia vishoka kwa ajili ya kuwatandazia nyaya majumbani mwao na badala yake watumie wakandarasi waliosajiliwa na Tanesco ili kuepuka kutapeliwa na kuingia hasara.

Alibainisha kuwa wapo wakandarasi wanaohusika na shughuli hiyo ya utandazaji nyaya (wiring) ambao wamesajiliwa kwa ajili ya shughuli hiyo. “Kabla ya kumpatia fundi shughuli ya kutandaza nyaya mnapaswa kujiridhisha kama anatambulika,” alisema.

Waziri Muhongo alimuagiza Meneja wa Tanesco mkoani humo, Mhandisi Masingija Lugata kuandaa orodha ya wakandarasi waliosajiliwa kwa ajili ya shughuli ya kutandaza nyaya  na kuisambaza kwenye Ofisi mbalimbali za Vijiji ili wananchi wapate kuwafahamu.

Alibainisha faida za kutumia wataalamu waliosajiliwa ambazo ni  pamoja na kuepuka kulipia gharama isiyostahili, kuepuka kutapeliwa na vilevile kuepuka kusababisha majanga yanayosababishwa na utandazaji duni wa nyaya za umeme kwenye maeneo yao.
...
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (mwenye fulana nyekundi) alipofika katika kijiji cha Bulombora Kigoma Vijijini kujionea moja ya eneo ambalo miundombinu ya umeme imeathirika kutokana na uchomaji wa misitu.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...