Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga  ameuagiza  uongozi wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), na Wakala wa Majengo Nchini (TBA), mkoa wa Kagera kufanya tathmini ya kina kwenye miundombinu ya barabara, madaraja na majengo ya Serikali yalioathirika na tetemeko la ardhi.

Eng. Nyamhanga ametoa agizo hilo Mkoani Kagera mara baada ya kukagua athari za tetemeko la ardhi katika barabara za Bukoba- Mtukula, Kyaka-Bugene na jengo la Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Tanzania na Uganda  ambapo amesema ni muhimu kufanya utafiti wa kitaalam katika miundombinu hiyo kabla ya hatua za ukarabati kuanza.

Amesema kufanyika kwa utafiti huo utasaidia kubaini athari nyingine zilizojificha ambazo zimetokana na tetemeko hilo.
“Undeni kikosi kazi cha wataalam maramoja waweze kuchunguza ili kujua sehemu mbalimbali zilizoathirika ili tuweze kuzitengeneza mapema iwezekanvyo”, amesema Eng. Nyamhanga.

Katika hatua nyingine Eng. Nyamhanga amemuagiza Mkandarasi wa Kampuni ya M/S China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) inayojenga barabara ya Kyaka-Bugeni (KM 59.1) kumaliza kipande cha Kilomita mbili katika barabara hiyo ifikapo mwezi Disemba mwaka huu.

Amesema kuwa kukamilika kwa kipande hicho kutaimarisha hali ya usafiri wa wananchi katika wilaya za Bukoba na Karagwe na hivyo kuhuisha shughuli za kiuchumi kwa wakazi wa Mkoa wa Kagera.
Eng. Nyamhanga yupo mkoani Kagera kukagua athari za uharibifu wa miundombinu kufuatia tetemeko la ardhi lililopiga mikoa ya Kagera, Mara na Mwanza Septemba 10 mwaka huu na kusababisha vifo vya watu takribani 17, majeruhi zaidi ya 100, uharibifu wa nyumba takribani 800 na miundombinu.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga (kushoto) akikagua sehemu ya barabara ya Bukoba-Mtukula ambayo imepata athari kutokana na tetemeko la ardhi lilitokea Mkoani Kagera hivi karibuni. Kushoto ni Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Mkoa wa Kagera Eng. Andrea Kasamwa.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga (kushoto), akitoa maelekezo kwa Meneja wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) Mkoa wa Kagera Eng. Andrea Kasamwa (kulia) wakati alipokagua Daraja la Kyaka katika Mto Kagera.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano (Sekta ya Ujenzi), Eng. Joseph Nyamhanga (wa pili kulia) akitoa maelekezo kwa Mkandarasi wa kampuni ya M/S China Henan International Cooperation Group Co. Ltd (CHICO) inayojenga barabara ya Kyaka-Bugeni (KM59.1), Mkoani Kagera.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...