Teresia Mhagama na Devotha Myombe

Tanzania imeahidi kuendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji katika Sekta ya Madini kama ilivyoainishwa katika Sera ya Madini ya mwaka 2009.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Profesa James Mdoe wakati wa semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji endelevu wa rasilimali madini nchini.

Alisema kuwa, Dira ya Maendeleo ya Mwaka 2025 imelenga katika kuanzisha migodi mikubwa, ya kati na midogo inayoendeshwa kwa kuzingatia usalama na utunzaji wa mazingira hivyo mazingira mazuri ya uwekezaji yatavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza ili kuendeleza Sekta ya Madini nchini.

Profesa Mdoe alisema kuwa semina hiyo ililenga katika kupata taarifa zilizohuishwa kutoka Japan na Tanzania kuhusu shughuli za utafiti na utunzaji wa mazingira katika Sekta ya Madini nchini na kujadiliana juu ya kuendeleza ushirikiano kati ya nchi husika.

“Semina hii ni muhimu kwani Taasisi hizi zitajadiliana kuhusu kuendeleza ushirikiano katika sekta hii, kufahamu fursa za uwekezaji kwenye Sekta ya Madini kwani wadau kutoka Tanzania na Japan wataweza kupata taarifa za utafiti kuhusu madini yaliyopo nchini na pia Taasisi ya JOGMEC itapata fursa ya kueleza shughuli zake barani Afrika,” alisema Profesa Mdoe.

Akieleza kuhusu Sekta ya Madini nchini, Profesa Mdoe alisema kuwa Sekta hiyo kwa sasa inachangia asilimia 3.5 katika Pato la Taifa na kueleza kuwa asilimia hiyo bado ni ndogo kwani lengo la Serikali ni kuona kuwa Sekta hiyo inachangia mpaka asilimia 10 kufikia mwaka 2025.

Hata hivyo Profesa Mdoe alisema kuwa ili sekta hiyo ichangie ipasavyo katika Uchumi wa Taifa, kutategemea kutoshuka kwa bei ya bidhaa zinazotokana rasilimali madini na uchumi wa dunia kuendelea kukua ili makampuni yanayojishughulisha na utafiti na uchimbaji wa madini yapate fedha kutoka Taasisi za kifedha duniani ili kuanzisha shughuli za utafiti na uchimbaji wa madini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (Katikati) akiwa katika picha ya pamoja na Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida (Wa pili kutoka kulia), Kaimu Kamishna wa Madini, Mhandisi Ally Samaje (Wa kwanza kushoto), Watendaji kutoka Serikali ya Japan na JOGMEC wakati wa semina iliyolenga katika uendelezaji endelevu wa rasilimali madini nchini.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe akifungua Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.
Balozi wa Japan nchini, Masaharu Yoshida (wa kwanza kulia) akimsikiliza Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia Madini, Profesa James Mdoe (hayupo pichani) akifungua Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.
Wadau mbalimbali waliohudhuria Semina iliyoandaliwa na Shirika la Umma kutoka Japan linalojishughulisha na Mafuta, Gesi na Metali (JOGMEC), Wizara ya Uchumi, Biashara na Viwanda ya Japan, Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), pamoja na Wizara ya Nishati na Madini iliyofanyika jijini Dar es Salaam iliyolenga katika uendelezaji Endelevu wa Rasilimali Madini nchini.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...