Muonekano wa mtambo wa kusaga kokoto katika kiwanda cha Kongolo cha TAZARA mkoani Mbeya unaotumika kutengeneza kokoto za kujaza tuta la reli.
Muonekano wa kokoto zinazosagwa na kiwanda cha Kongolo cha TAZARA mkoani Mbeya zinazotumika katika uimarishaji wa tuta la reli.
Baadhi ya nondo zinazotumika kutengeneza mataruma katika kiwanda cha Kongolo cha TAZARA Mkoani Mbeya.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

WAKATI Serikali ikiwa katika hatua za kumpata mkandarasi wa ujenzi wa reli ya kisasa nchini (Standard Gauge), Mamlaka ya reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) imesema imewasilisha andiko kwa Kampuni miliki ya rasilimali za Reli (RAHCO) ili kuanza utengenezaji wa mataruma na uzalishaji wa kokoto zitakazotumika kwenye ujenzi wa reli hiyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mhandisi Mzalishaji wa kiwanda cha kuzalisha mataruma cha TAZARA mkoani Mbeya, Eng. Boniface Phiri ikiwa ni siku chache baada ya RAHCO kutangaza zabuni hiyo ambapo amesema kuwa kiwanda hicho kina uwezo mkubwa wa kuzalisha mataruma kwa ajili ya ujenzi wa mradi huo.

Eng. Phiri amesema pamoja na agizo la Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano alilolitoa kwa mamlaka hiyo Mwezi mmoja uliopita alipotembelea kiwanda hicho na kuelekeza kuwa Mamlaka ijipange kuzalisha mataruma na kokoto.

“Mamlaka imejitathmini na kuona kwamba kutokana na uwezo tulionao tumeshawasilisha andiko letu kwa RAHCO na tunasubiri majibu yao ili kuanza kazi ya uzalishaji”, amesema Eng. Phiri.

Amebainisha kuwa kwa sasa Mamlaka inaboresha mitambo na kuangalia namna ya kuanza kutumia teknolojia ya mvuke kwenye uzalishaji ili kuongeza idadi ya mataruma na  ubora unaokidhi viwango ambapo kwa siku kiwanda huzalisha mataruma zaidi ya 200.

Aidha Eng.Phiri ameishukuru Serikali Ya Tanzania na Zambia kwa kuisadia Mamlaka hiyo tani 300 za nondo ambazo zimesaidia kuongeza uzalishaji wa mataruma katika kiwanda.

Kwa upande wake Mhandisi Mzalishaji wa mgodi wa kokoto Eng. Juma Mizambwa amesema uzalishaji wa mataruma unaenda sambamba na uzalishaji wa kokoto ambapo kwa sasa mgodi huo unazalisha tani 180 kwa siku.

Mradi wa ujenzi wa Reli ya Kisasa unatarajiwa kuanza Mwezi Desemba mwaka huu ambapo kwa mwaka wa fedha 2016/17 Serikali imetenga shillingi Trilioni moja kwa ajili ya utekelezaji wake.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...