Mkuu wa Wilaya
ya Arusha Mjini Mh. Gabriel Fabian Daqarro amelipongeza Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuendesha mafunzo maalum kwa waandishi wa Habari wa
Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara.
Mh. Gabriel
Daqarro ameyasema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya siku moja ambayo
yamefanyika Septemba 19 katika ukumbi wa Chuo cha Afya CEDHA mkoani Arusha.
“Ingawa mafunzo
ni mafupi lakini napenda kulipongeza Shirika letu la Mafuta la Taifa kwa kuona
umuhimu wa vyombo vya habari katika kupata uelewa mpana wa Sekta Ndogo ya
Mafuta na Gesi ili waweze kuhabarisha na kuelimisha watanzania kwa ujumla ili
watambue shughuli za shirika na faida zake haswa katika uchumi wa nchi”,
alieleza Mkuu wa Wilaya.
Aidha Mh.
Daqarro amewaomba Waandishi wa Habari kuwa wazelendo katika kuisaidia Serikali
kutekeleza miradi mbalimbali yenye maslahi mapana katika maendeleo ya nchi
yetu. ‘’Waandishi Wahabari mnapaswa kuisaidia Serikali katika utekelezaji wa
miradi mbalimbali yenye tija kwa uchumi wa Taifa, mfano katika vita ya kiuchumi
ya kugombania mradi wa bomba la mafuta ghafi kutoka Uganda kati ya Tanzania na
Kenya, wenzetu Kenya walijitahidi kuandika habari zenye kutoa wasifu wa nchi
yao ili kuisaidia kupata mradi huo, hivi ndivyo mnavyopaswa kufanya kazi
kiuzalendo.”
Aliongeza kuwa “leo
hii mmeweza kuifahamu TPDC sasa mnapaswa kuwaeleza wananchi miradi inayofanywa
na Shirirka hili na manufaa yake katika uchumi wa Taifa, mwende mkatafiti namna
mradi wa bomba la mafuta utakavyonufaisha wananchi wanaoishi kando ya njia ya
bomba hilo, vilevile namna bomba hilo litakavyosaidia kukuza uchumi wa nchi,
hivi ndivyo tunavyoweza kujenga nchi yetu kupitia taaluma ya uandishi wa habari.”
Mkuu wa Wilaya
alisisitiza kuwa ili tujenge Taifa imara ni vyema tuandike habari kwa weledi,
uzalendo huku tukiondoa tofauti zetu za kiitikadi ziwe za kikabila, kisiasa au
kidini kwa namna hii tutaweza kuandika habari zenye kujenga nchi yetu na si
vinginevyo.
Hata hivyo
Mwenyekiti wa Waandishi wa Habari Arusha ndugu ….pamoja na dhamira ya dhati ya
Shirika katika utoaji wa elimu ya sekta ameliomba TPDC kutenga muda wa kutosha
zaidi katika uelimishaji ili walengwa waweze kuelewa vyema sekta, ombi ambalo liliungwa
mkono na Mkuu wa Wilaya.
Katika mafunzo
hayo waandishi wa habari walipata fursa ya kujifunza kuhusu maendeleo ya Sekta
Ndogo ya Mafuta na Gesi, Matumizi ya Gesi Asilia na Faida Zake, Mradi wa Bomba
la Kusafirisha Mafuta Ghafi kutoka Uganda hadi Tanga na Usambazaji wa Gesi
Asilia Majumbani, Viwandani na kwenye Vituo vya Kujaza Magari.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini Mh. Gabriel
Fabian Daqarro akisisitiza umuhimu wa Waandishi wa Habari nchini katika kujenga
uchumi wa nchi pale wanapotumia kalamu na taaluma yao kuelezea miradi
inayotekelezwa na Serikali kwa maslahi ya taifa.
Mwanasheria wa
TPDC ndg Goodluck Shirima akitoa mada ya Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka
Uganda hadi Tanga kwa Waandishi wa Habari wa Mikoa ya Arusha, Manyara na
Kilimanjaro.
Waandishi
wa Habari wa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara wakipata mafunzo ya
masuala ya Mafuta na Gesi yaliyoandaliwa na TPDC.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...