Wananchi waliokumbwa na tetemeko la ardhi mkoani Kagera na nyumba zao kuathiriwa, wameaswa  kutokuanza ujenzi wa nyumba hizo  hadi hapo wataalam watakapotembelea maeneo yao na kuwapatia ushauri kuhusu ujenzi husika.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo wakati alipofanya ziara mkoani humo ili kukagua shughuli za utafiti wa tetemeko zinazoendelea kufanywa na wataalam kutoka Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST) kwa kushirikiana na wataalam kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.

Katika ziara hiyo, Waziri Muhongo alizungumza na wananchi ambao walitaka kufahamu kitaalam kama wanaweza kuendelea kujenga nyumba zao ambazo ziliathiriwa na tetemeko hilo.

"Nyumba zetu zimeathiriwa na tetemeko na hatujaanza kurekebisha; Je kitaalam tunaweza kuziendeleza?,"aliuliza mmoja wa wananchi.

Akijibu swali hilo, Waziri Muhongo aliwaasa wananchi hao kuwa na subira ili wataalam wakague Nyumba zao na kuwashauri kabla ya kuendelea na hatua ya ujenzi  na wakati huohuo aliwaagiza wataalamu hao ambao wako mkoani humo kufanya zoezi hilo haraka.

"Ni vyema mkawa na subira kabla hamjafanya kitu ili wataalam wapite kufanya ukaguzi pamoja na kuwapatia ushauri wa kitaalam, " alisema Profesa Muhongo.

Aidha, Waziri Muhongo aliwataka wananchi hao kuepuka kusikiliza kauli za watu wasiokuwa wataalam kuhusu tetemeko hilo na badala yake aliwaasa wananchi hao  wafuatilie ushauri wa wataalam wanaoendelea na shughuli za utafiti katika maeneo yaliyoathiriwa na tetemeko la ardhi mkoani humo.

Kutokana na maswali mbalimbali aliyokuwa akiulizwa na wananchi katika maeneo aliyotembelea, Waziri Muhongo alimuagiza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania (GST), Profesa Abdulkarim Mruma kutoa namba yake ya simu ili wananchi watakaokuwa na maswali yoyote yatakayojitokeza ama endapo kutatokea hali ambayo hawaielewi waweze kuwasiliana nae.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akimsikiliza mkazi wa Kijiji cha Kigazi, John Kilibwa akiuliza maswali kuhusiana na Tetemeko.
Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo (kushoto) akijadiliana jambo na Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Jiolojia Tanzania, Profesa Abdulkarim Mruma wakati wa ukaguzi wa shughuli za utafiti wa Tetemeko la ardhi, mkoani Kagera.
Moja ya nyumba ambazo zimeathirika kutokana na Tetemeko la ardhi lililotokea mkoani Kagera.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...