THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

UVCCM YAWAVUA KATIBU NA MWENYEKITI ARUSHA

KAMATI ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Taifa, limependekeza kwa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CC) kumvua uongozi Mwenyekiti wa umoja huo mkoani Arusha, Lengai Ole Sabaya, kwa tuhuma mbalimbali ikiwemo kufikishwa mahakamani akituhumiwa kwa utapeli. 

“Wakati tukisubiria uamuzi wa Chama, Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa imemsimamisha uongozi wa nafasi yake ndani ya UVCCM kutokana na kesi iliyoko Mahakamani na kumtaka kuanzia leo (jana) asijihusishe na shughuli zozote za uongozi wa UVCCM hadi hatima ya tuhuma zake itakapoamuliwa na Mahakama na vikao husika vya UVCCM na CCM. 

Mbali na Sabaya, UVCCM pia imemtimua kazi aliyekuwa katibu wake mkoani humo kwa kukiuka utaratibu na maagizo ya UVCCM na CCM ikiwemo vitendo vya utovu wa nidhamu. 

Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana Dar es Salaam na kutiwa saini na Kaimu Katibu Mkuu wa UVCCM, Shaka Hamdu Shaka, ilisema Kamati ya Utekelezaji ya Baraza Kuu la UVCCM Taifa ilikutana Septemba 19, nwaka huu Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Sadifa Juma Khamis ambapo pamoja na mambo mengine walifikia uamuzi huo. 

Ilisema kikao hicho kilitanguliwa na kikao cha Kamati ya Maadili na Nidhamu ya UVCCM Taifa, ambapo pamoja na mambo mengine kilipokea na kujadili uhai wa CCM na umoja huo mkoani Arusha. Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo walijadili kuyatolea ufafanuzi mambo mbalimbali kuhusu makada wake hao wawili. 

Taarifa ya Shaka ilisema miongoni mwa mambo yaliyomhusu Sabaya ikiwemo kuyaongoza makundi ya vijana wa CCM na wasiokuwa wa CCM ili kumkataa Katibu wa UVCCM aliyehamishiwa mkoani Arusha, Said Goha kuchukua nafasi ya Ezekiel Mollel. Ilisema kuwa Sabaya licha ya kupewa heshima na kuelimishwa na vikao vya juu na viongozi mara kwa mara kupitia Mwenyekiti wa UVCCM taifa, kuhusu mamlaka za kikanuni ikiwemo ya utumishi na maadili ya UVCCM lakini ameshindwa kujirekebisha. 

“Sabaya amesababisha taharuki iliyosababisha ofisi za UVCCM Arusha kufungwa kwa minyororo hadi Jeshi la Polisi kuingilia kati. Vile vile taharuki hiyo imechangia kwa kiasi kikubwa Vijana wa mkoa wa Arusha kugawanyika katika makundi na kusababisha hali ya usalama na maadili kwa umoja huo na Chama kuwa ya wasiwasi. 

“Sabaya kufikishwa mahakamani akikabiliwa na mashitaka mawili likiwemo la kujifanya mtumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa. Huku kosa la pili katika muda usiojulikana akidaiwa kughushi vitambulisho vya Idara ya Usalama wa Taifa (TISS) chenye namba MT 86117 wakati akijua ni kinyume cha Sheria za nchi. 

“Kamati ya Utekelezaji ilipitia tuhuma mbalimbali na vielelezo vya utapeli na ulaghai unaodaiwa kutendwa na Sabaya katika maeneo tofauti huku akijua ni kinyume na miiko na maadili ya uongozi wa UVCCM na CCM.
“Kwa makosa yote hayo Sabaya amekukiuka kanuni ya uongozi na maadili ya CCM Fungu la (3) ukurasa wa 16 na 17, na fungu la (4) ukurasa wa 29, 30 na 31. Pia makosa hayo ameyatenda kinyume na utaratibu wa uongozi na maadili ya UVCCM, Ibara ya 6.3.2 Ibara ya 7.5.1, 7.5.4 na 8.2.5,”alisema.