Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani akiwasili nyumbani kwa familia ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Butiama Musoma akiwa ameambatana na watumishi wa NEC na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa ALAT kutoka maeneo mbalimbali kuzuru kaburi la Baba wa Taifa, Mwitongo wilayani Butiama. Tume ya Taifa ya Uchaguzi iko mkoani Mara kutoa elimu ya mpiga kura kwa wananchi. 

Na. Aron Msigwa – NEC, Musoma.

Viongozi wa vyama vya Siasa wametakiwa kuiga kwa vitendo uzalendo na moyo wa kujitoa aliokuwa nao Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere enzi za uhai wake ili kuliwezesha Taifa kupiga hatua kimaendeleo.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Bw. Kailima Ramadhani mara baada kutembelea Kaburi na Makumbusho ya Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo wilayani Butiama.

Amesema kuwa kumbukumbu za Baba wa Taifa zilizohifadhiwa vizuri katika makumbusho hiyo zina mambo mengi ya kujifunza ambayo wanasiasa wanatakiwa kuyafanya kwa vitendo hasa uzalendo kwa nchi, uvumilivu, upendo na moyo wa kujitoa kwa dhati kuwatumikia wananchi.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani (Kushoto) akisalimiana na Msemaji Mkuu na kiongozi wa familia ya Baba wa Taifa Chifu Japhet Wanzagi (kulia) mara baada ya kuwasili eneo la Mwitongo wilayani Butiama. Wa Pili kutoka Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya Butiama Bi. Annarose Nyamubi.

“Kupitia kumbukumbu hizi sisi watumishi wa Tume tumejifunza ukomavu wa demokrasia aliokuwa nao Mwalimu Nyerere akiwa ndani na nje ya Bara la Afrika, wengi wanadhani Demokrasia ni wakati wa uchaguzi tu, kumbe demokrasia ni pamoja na kuheshimu watu wengine” Amesema Kailima.

Ameeleza kuwa maisha aliyoishi Baba wa Taifa ni mfano wa kuigwa na viongozi na watanzania wote hasa pale alipojitofautisha na viongozi wengi wa Bara la Afrika alipoepuka tamaa ya madaraka na mali kwa manufaa ya taifa.

“Sote ni mashahidi kupitia kumbukumbu zake tumeona mahali alipokuwa anaishi mwalimu Nyerere kabla hajajengewa nyumba na Jeshi, kama Rais mstaafu wengi walitegemea asingeishi katika eneo lile, kumbukumbu hii nzuri aliyoiacha inatufundisha watanzania kuwa mwalimu aliitanguliza Tanzania mbele kuliko maslahi yake binafsi” Amesisitiza Kailima.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Kailima Ramadhani akiwasha mshumaa kwenye kaburi la Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere eneo la Mwitongo, Butiama. Wengine wanaoonekana na baadhi ya wajumbe wa mkutano wa ALAT na watumishi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


Bw. Kailima amebainisha kuwa NEC itaendelea kumuemzi Baba wa Taifa kwa yale aliyoyafanya na kuyasimamia kwa manufaa ya taifa huku akitoa wito kwa viongozi wa vyama vya Siasa wawe na kiasi na waridhike na vile walivyonavyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...