Meneja wa Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshack Bandawe akizungumza na wanachama wa mfuko huo jijini Mwanza jana kabla ya kuwakabidhi kadi za matibabu ya mfumo wa uchangiaji wa hiari(Wote Scheme).

Na Baltazar Mashaka,Mwanza

WANACHAMA 106 kati ya 7, 185 wa Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa kupitia mfumo maalum wa uchangiaji wa hiari wa WOTE Scheme wamekabidhiwa kadi zitakazo wawezesha kupata huduma za matibabu.

Akikabidhi kadi hizo kwa wanachama hao, Meneja wa PPF Kanda ya Ziwa Meshach Bandawe alisema mfumo huo umewalenga wanachama waliojiajiri wenyewe katika Sekta isiyo rasmi ambao kwa mujibu wa takwimu za kitaifa ni zaidi ya asilimia  90 ya nguvu kazi ya taifa.

Alisema kuwa bahati mbaya kundi hilo lilisahaulika na halijakingwa kikamilifu na sekta ya Hifadhi ya Jamii nchini ingawa ni ukweli usiopingika kuwa wanapatwa na majanga hatarishi sawa na wafanyakazi wa sekta rasmi.

“ Watu waliojiajiri kwenye Sekta isiyo rasmi wanafanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na uzalishaji mali  na kuwaingizia kipato cha uhakika na kumudu kuendesha maisha yao.Bahati mbaya hawana akiba yoyote wanayoweza kunufaika nayo kwa maisha ya baadaye iwapo wangejiunga na mifuko ya Hifadhi ya Jamii,” alisema.
Meneja wa Mfuko wa Pensheni wa PPF Kanda ya Ziwa, Meshack Bandawe akimkabidhi Anastanzia Magere kadi ya matibabu ya mfumo wa uchangiaji wa hiari(Wote Scheme) jijini Mwanza jana. Mpaka sasa Kanda hiyo wamekwishajiunga wanachama 7185 kwa kipindi cha Agosti 2015 mpaka Agosti 2016. Picha na Lordrick Ngowi

Meneja huyo wa PPF alieleza kuwa mfuko kwa kushirikiana na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya ( NHIF) utatoa huduma ya matibabu kwa wanachama baada ya kuchangia sh.60,000  na watatibiwa magonjwa yaliyoanishwa kwenye sera ya kitaifa.

Bandawe alisema wanachama hao watapata huduma hiyo ya matibabu katika hospitali zaidi ya 6,000 nchini ambazo zimeingia mkataba na NHIF na wanastahili kuwa na kadi watakazotumia kupata huduma hizo kwa kipindi cha mwaka mmoja na akatoa wito kwa makundi mbalimbali yaliyoko katika sekta isiyo rasmi yajiunge na mfumo huu kwa faida ya maisha yao na wanufaike na huduma mbalimbali zinazotolewa na PPF .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...