Hususani kuhusu uondoaji wa wafanyakazi hewa, sera ya elimu bure na usimamishwaji wa watumishi wa serikali kutokana na makosa mbalimbali. 
uondoaji wa wafanyakazi hewa ulitajwa na asilimia 69 ya wananchi wa Tanzania, kama juhudi mojawapo ya Rais John Pombe Magufuli, wanayoifurahia sana.

 Elimu bure (asilimia 67) na usimamishwaji wa watumishi wa serikali (asilimia 61) navyo pia vilishika nafasi za juu. Walipoambiwa wataje vitendo ambavyo hawakubaliani navyo, asilimia 32 walitaja kuzuiliwa kwa uagizwaji wa sukari na bei elekezi ya sukari. 

Hatahivyo, asilimia 58 hawapingi kitendo chochote cha Rais. Kwa ujumla kiwango cha kukubalika kwa Rais Magufuli anakubalika na asilimia 96 ya wananchi. Kiwango hiki kinaendana na viwango vya kukubalika kwa marais wa Tanzania waliopita.

Pamoja na hayo, asilimia 88 ya wananchi wana imani kuwa Rais Magufuli ataendelea na kasi aliyoanza nayo, mpaka mwisho wa awamu yake ya uongozi.

Viwango vya kukubalika vya viongozi wengine wa serikali pia vipo juu  Wananchi wanaonekana kumkubali mwenyekiti wao wa kijiji/mtaa (asilimia 78), diwani wao (asilimia 74) na mbunge wao (asilimia 68).

Matokeo haya yametolewa na Twaweza kwenye utafiti uitwao Rais wa Watu? Tathmini na matarajio ya wananchi kwa serikali ya awamu ya tano. Muhtasari huu unatokana na takwimu kutoka Sauti za Wananchi, ambao ni utafiti wa kwanza barani Afrika wenye uwakilishi wa kitaifa unaotumia simu za mikononi. Matokeo haya yanatokana na takwimu zilizokusanywa kutoka kwa wahojiwa 1,813 kutoka maeneo yote Tanzania Bara (Zanzibar haihusiki kwenye matokeo haya) kati ya tarehe 4 Juni na tarehe 20 Juni 2016. 

Wananchi wengi wanasema serikali ya awamu ya tano imeleta maboresho kwenye huduma nyingi za umma. Inayoongoza ni Mamlaka ya Mapato Tanzania ambapo asilimia 85 ya wananchi wanasema huduma zimeboreshwa chini ya serikali mpya. Wananchi pia wanasema huduma ni nzuri mashuleni (asilimia 75), vituo vya polisi (asilimia 74), mahakamani (asilimia 73), vituo vya afya (asilimia 72) na mamlaka za maji (asilimia 67). Ni vema ikafahamika kuwa takwimu hizi zinaonyesha mitazamo na maoni ya wananchi kuhusu huduma za umma na siyo lazima ikawa ndiyo hali halisi ya mabadiliko kwenye huduma hizo. Vilevile, karibu wananchi wote (asilimia 95) wanasema watumishi wa umma wanaotoa huduma, kama madaktari, walimu, pamoja na maofisa tawala wa umma wamekuwa wakiwajibika zaidi.

Hata hivyo, wananchi wenyewe wanakubali kuwa hawapati taarifa za kutosha kuhusu masuala muhimu ya kitaifa. Ni asilimia 4 tu wanaosema wanapata taarifa za kutosha kuhusu masuala ya siasa nchini na asilimia 9 tu wanasema wanapata taarifa kuhusu masuala yanayohusu afya na elimu. Hii inamaanisha kuwa maboresho yanayosemwa kuhusu huduma za umma yanatokana na uzoefu binafsi au kutoka vyanzo visivyo rasmi. Hatahivyo, wananchi wanatamani kupata taarifa kutoka katika sekta ambazo zinagusa maisha yao. Walipoulizwa masuala gani wangependa kumuuliza mwenyekiti wao wa kijiji, diwani au mbunge, masuala yanayohusu afya, elimu, maji na barabara yalijitokeza kama mambo muhimu. Kwa upande wa Rais Magufuli, wananchi wawili kati ya kumi (asilimia 18) wangependa kumuuliza kuhusu suala la mfumuko wa bei kwa bidhaa mbali mbali.

Mwenendo unaofanana umejitokeza pale wananchi walipoulizwa iwapo wanamfahamu au wameshazungumza na viongozi wao wa vijiji, wilaya na kitaifa. Karibu wananchi wote (asilimia 96) waliripoti kumfahamu Afisa Mtendaji wa Kijiji chao na karibu nusu yao (asilimia 47) walikuwa wameshawahi kuzungumza naye. Hatahivyo, asilimia 21 ya wananchi wanamfahamu Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya yao na asilimia 4 pekee wamezungumza naye.

Pamoja na kiwango kikubwa cha kukubalika kwa serikali ya awamu ya tano na Rais John Pombe Magufuli, wananchi wapo makini na kanuni za demokrasia na haki na wanataka zifuatwe. Wananchi nane kati ya kumi (au 80%) wanasema watendaji wa umma waondolewe pale tu panapokuwepo udhibitisho wa vitendo viovu. Asilimia 75 wanasema kuwa watendaji waondolewe pale wanaposhindwa kufanya kazi zao na siyo wanaposhindwa kufuata maagizo ya Rais. Pamoja na shauku yao juu ya uondoaji wa watumishi wa umma, wananchi wana maoni tofauti kuhusu matokeo ya kuwaondoa watumishi wa umma. Japokuwa asilimia 90 wanasema uondoaji wa watumishi hawa utawafanya watumishi wengine kuepuka vitendo viovu, asilimia 37 wanasema itawapunguzia morali watumishi wengine. Asilimia 48 wanasema uondoaji wa watumishi utawasababishia watumishi kutafuta njia mpya za kuficha maovu.

“Wananchi wana mitazamo chanya kuhusu utendaji wa serikali ya awamu ya tano pamoja na Rais Magufuli mwenyewe. Wanasema kuwa watumishi wa umma kwenye maeneo mbalimbali wanawajibika zaidi na kwamba wamegundua kuwa kuna maboresho kwenye huduma za umma. Hata hivyo wananchi wana mashaka kuhusu utaratibu unaotakiwa kufuatwa. Kwa mfano, wanataka udhibitisho wa vitendo viovu upatikane kwanza kabla ya watendaji kuwajibishwa, kulaumiwa ama kutiwa aibu. Vilevile wana mashaka kuhusu maamuzi ambayo yanaweza kugharimu fedha zao, kama kuzuia uingizwaji wa sukari. Hii inaonyesha kuwa wananchi hawatakuwa wakikubaliana na vitendo vyote vinavyofanywa na Rais bila kuhoji. Wananchi wanaendelea kuthamini  misingi ya utawala bora unaozingatia sharia zilizopo,’ anasema Mkurugenzi Mtendaji wa Twaweza, Aidan Eyakuze.

“Jambo muhimu kuhusu matokeo haya” anaendelea Bwana Eyakuze, “ni kuwa matarajio ya wananchi yamebadilika. Kipindi cha nyuma kulikuwa na hali ya kutokujali miongoni mwa wananchi, uzoefu uliotokana na utendaji duni uliodidimiza matarajio yao, na matokeo yake yakichangia utendaji usioridhisha kuendelea. Lakini mabadiliko tunayoyaona hivi sasa yanaonyesha kuwa utendaji wa sekta ya umma unaweza kuimarika. Wananchi wanaweza kutarajia viwango vya juu zaidi kama utaratibu huu mpya ni wa kudumu.”

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...