Na Mwandishi Maalum, New York

Tanzania imeitaka jumuiya ya kimataifa kujadili tatizo la uwepo wa watu ambao si raia wa nchi yoyote ile.

Pendekezo hilo limetolewa siku ya Jumanne na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga ( Mb) katika mkutano wa Kilele wa viongozi kuhusu wakimbizi.

Mkutano huo uliandaliwa na Rais wa Marekani Barack Obama kwa ubia na nchi za Ethiopia, Jordan, Mexico, Sweden, Canada na Ujerumani ambapo nchi 60 zilialikwa,45 kati ya zilizoalikwa ikiwamo Tanzania zilitoa ahadi ya namna moja ama nyingine. Nchi hizo ni zile ambazo kwa namna moja ama nyingine zimekuwa zikiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi, zimekuwa nchi za mpito kwa wakimbizi, au zimekuwa zikitoa misaada ikiwamo ya hali na mali pamoja na kuwapatia uraia, ajira na misaada ya kibinadamu.

Lengo kuu la mkutano huo wa viongozi kuhusu wakimbizi lilikuwa ni kwa nchi kutoa ahadi mpya ambazo kwayo zitasaidia katika kuwapatia fursa za ziada wakimbizi ili pamoja na mambo mengine kuwapunguzia changamoto zinazowakabili na kuwafanya wajisikie na kujiona kuwa nao ni binadamua kama binadamu wengine.

Akizungumza kwa niaba ya Serikali, Waziri Mahiga, amesema, Tanzania kutokana na jiografia ya nchi hiyo ilivyo imejikuta mara kwa mara ikiwa ni kimbilio la wakimbizi kutoka nchi jirani.

Akawaeleza washiriki wa mkutano huo, kwamba, suala la Tanzania kuwahifadhi wakimbizi ni la kihistoria na halikuanza jana au juzi.
“ Tanzania kutokana na jiografia yake imejikuta ikiwa ni kimbilio wa watu wanaotafuta salama ya maisha yao. Tumekuwa tukiwapokea na kuwahifadhi wakimbizi tangu miaka ya 60. Na tunatekeleza jukumu hilo kwa kuzingatia sheria za kimataifa na mikataba ya kimataifa, na sheria zetu za ndani” akasema Mahiga. Na kuongeza kwamba, Tanzania itaendelea na jukumu hilo pale itakapopashwa kufanya hivyo kwa kufuata na kuzingatia sheria za nchi na sheria za kimataifa.

“Tumekuwa tukitiliza mkazo na kujadili mara kwa mara tatizo la wakimbizi na changamoto wanazokabiliana nazo. Na mshukuru Rais Obama kwa kuitisha mkutano huu. Lakini kuna jambo jingine muhimu na ambalo tunatakiwa tulijadili pia . Na hili linahusu uwepo na kuendelea kuongeza wa idadi ya watu hususani vijana ambao hawana uraia wa nchi yoyote ile ( stateless people).

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki akielezea zaidi kuhusu changamoto hiyo ya uwepo wa watu ambao hawana uraia wa nchi yoyote ile. Amesema tatizo hilo linaonekana zaidi katika eneo la Kusini na Eneo la Maziwa Makuu.

“ Tunapo jadili namna ya kuwasaidia wakimbizi, ni vema pia tukatambua kwamba kuna tatizo kubwa la uwepo wa watu ambao hawajasajiliwa na hawana uraia wa nchi yoyote. Na tatizo hili ni kubwa na linazindi kuongezeka na lipo zaidi kwa kizazi cha sasa, hawana uraia. Tunatakiwa kulijadili tatizo hili”. Akasisitiza Waziri Mahiga. Na kubainisha kuwa Tanzania, ikiwa ni mwanachana wa SADC na EAC itaangalia uwezekano wakuipekea mezani ajenda hiyo kupita Taasisi hizo mbili.

Kwa pande wa ahadi za ama nini zaidi Tanzania itawafanyia wakimbizi , Waziri amesema pamoja na ahadi ya kuendelea kuwapokea wakimbizi pale inapobidi kufanya hivyo, Tanzania pia kupitia sheria zake itawasaidia watoto wakimbizi kupata huduma za jamii zikiwamo za elimu na afya, na kwa wakubwa fursa za kujiajili hususani katika sekta ya kilimo iliwe waweze kuzalisha chakula na kujiajili kupitia kilimo. Ahadi nyingine ni pamoja na kutowarudisha kwa nguvu wakimbizi katika nchi walizotoka.

Katika mkutano huo ambazo uongozi wa Juu wa Serikali ya Obama ulikuwapo kuanzia Makamu wake Joe Biden na Waziri wa Mambo ya Nje John Kerry, Rais Obama kwa upande wake alitoa ahadi za kuongeza idadi ya wakimbizi watakaoingia nchini Marekani pamoja na kuongeza misaada ya kifedha kwaajili ya misaada na huduma za kijamii pamoja na kuzisaidia nchi zinazobeba mzigo wa wakimbizi.

Barack Obama ambaye anaelekea ukingoni mwa uongozi wake, amesema jumuiya ya kimataifa haipashwi kufanya kazi kwa mazoea na hasa katika eneo hilo la wakimbizi eneo ambalo anasema linahitaji ushiriki na ushirikiano wa kila nchi bila ya kujali ukubwa au udogo wake,ajiri au umaskini wake. Mkutano huo mbali ya Marais, Wafalme, Mawaziri Wakuu na Mawaziri kuzungumza pia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa naye alizungumza pamoja nna Mkuu wa Banki ya Dunia.

Ni mkutano ambao ulikuwa ni mwendelezo wa majadiliano ambayo yalifanyika siku ya Jumatatu kuhusu ajenda ya wakimbizi na wahamiaji kama changamoto ya dunia hivi sasa. Licha ya machafuko na vita, suala ya umaskini, uongozi mbovu na watu kutokuwa na matumaini ni maeneo ambayo yameelezwa kuchangia katika uongezeko la wakimibizi.

Pamoja na kuandaa na kushiriki mkutano wa viongozi kuhusu wakimbizi, Rais wa Marekani Barack Obama siku hiyo ya jumanne alilihutubia kwa mara ya mwisho Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa, ambapo aliainisha masuala mbalimbali yanayoikabili dunia hivi sasa yakiwamo ya ugaidi, mabadiliko ya tabia nchi, ukiukwaji wa haki za binadamu, ukiukwaji wa utawala wa sheria na demokrasi, milipuko ya magonjwa kama vile Ebola na Zika, matumizi ya diplomasia katika kutafutia ufumbuzi masuala magumu likiwamo la mchakato wa kuidhibiti Iran dhidi ya silaha za nyukilia.
Pamoja na kuhudhuria siku ya kwanza ya ufunguzi wa Baraza Kuu la 71 la Umoja wa Mataifa, Kiongozi wa Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huu pia alipata nafasi na fursa ya kuwa na mazungumzo na baadhi ya viongozi. Pichani Waziri Mahiga akibadilishana mawazo na Katibu Mkuu Mtendaji wa SADC Dr. Stergomena Tax .
Waziri Mahinga pia alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi Bw. Alain Nyamwitwe

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...