Mwandishi wetu, Mwanza

Chacha Masinde kutoka mkoani Mara ameibuka mshindi wa kwanza kwenye mbio za Rock City Marathon zilizofanyika jana jijini Mwanza baada ya kumaliza kwa muda wa saa 01:03:00, akifuatiwa na mshiriki kutoka nchini Kenya David Kilimo aliyetumia muda wa saa 01:04:40

Mbio hizo za kilomita 21 zilianzia Uwanja wa CCM Kirumba kupitia Barabara ya ikulu ndogo hadi mzunguko wa samaki na kuelekea Buzuruga kisha kutokea barabara ya pasiansi na kumalizikia uwanjani Kirumba huku Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Bw John Mongella akishiriki kukimbia mbio za km 5 sambamba na watu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino.

Nafasi ya tatu upande wa wanaume ilichukuliwa na Mkenya Moris Mosima aliyetumia muda wa saa 01:04:57, ikiwa sekunde chache nyuma ya mpinzani wake.

Akizungumzia siri ya ushindi wake, Chacha siri ya mafanikio hayo ni kujituma kwake zaidi katika kufanya mazoezi maalum kwa ajili ya mashindano hayo ili kuhakikisha kwamba mwaka huu mshindi wa kwanza katika mbio hizo anatoka nchini Tanzania tofauti na miaka ya nyuma ambapo washindi walikuwa wakitoka nchini Kenya.

“Niliweka nadhiri nikasema mwaka huu lazima mshindi atoke Tanzania zaidi niwe mimi na ninashukuru nimetimiza adhama yangu. Pamoja na hilo maandalizi ya mwaka huu yamekuwa mazuri zaidi mahitaji yote muhimu yakiwemo maji tukiwa njiani yamesaidia mafanakinio hayo licha ya washiriki kuwa zaidi mwaka huu hatua ambayo iliongeza changamoto kwetu zaidi,’’ alisema.

Upande wa wanawake mshindi wa kwanza ni Mtanzania pia Faimina Abdi kutoka mkoani Arusha aliyetumia muda wa saa 01:13:12 akifuatiwa na mwenzake kutoka mkoani Arusha Angelina Daniel aliyetumia saa 01:14:38 huku Mkenya Dorifine Omary akishika nafasi ya tatu akitumia saa 01:16:54

Washindi wa kwanza katika mbio hizo zilizofanyika kwa mara ya nane jijini Mwanza waliibuka na kitita cha Sh1.5 milioni kila mmoja, washindi wa pili Sh900,000 na washindi watatu Sh700,000.

Mashindano hayo ya kila mwaka yaliyokatika kalenda ya RT yaliandaliwa na Kampuni ya Capital Plus kwa udhamini kampuni za Freidkin Conservation Fund na African Wildlife Trust, Benki ya NMB, New Mwanza Hotel, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Real PR Solutions, kampuni ya Fabec, Tiper, Puma Energies, Clouds Fm, Jembe Fm, Barmedas Tv na EF Out Door.

Akizungumza kabla ya kukabidhi zawadi kwa washindi kwa washindi na washiriki wa wa mbio hizo Mkuu wa mkoa wa Mwanza, Bw John Mongella ambae pia alishiriki mbio hizo kwa kukimbia mbio za km 5 alisema mbio hizo ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa wanariadha nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuirudishia nchi heshima yake katika mchezo huo.

“Ndio maana tumekuwa tukisisitiza wadhamini waendelee kujitokeza kusaidia mbio hizi ili ziendelee kuwa bora zaidi,’’ aliongeza.

Akikabidhi zawadi kwa washindi wa mbio hizo kwenye uwanja wa CCM Kirumba kwa niaba ya Katibu tawala jana, Afisa michezo mkoa waMwanza James William alisema mbio hizo ni nyenzo muhimu ya kuwaandaa wanariadha wetu nchini kuwa katika nafasi ya kufanya vizuri katika michuano ya kimataifa na kuirudishia nchi yetu heshima ya kipekee katika mchezo huo kama ilivyokuwa miaka ya nyuma.

Alisema: “Tanzania inaweza kurejea katika ramani ya dunia kwenye michezo kama tukijikita katika maandalizi mazuri ya kuibua na kuviendeleza vipaji vya vijana wetu nchini hasa kuanzia ngazi ya shule za msingi.”

Naye Mbunge wa jimbo la Ilemema ambae pia ni Naibu Waziri Wizara ya Ardhi, Ntumba na Maendeleo ya Makazi Bi Angelina Mabula alipongeza waandaaji wambio hizo na kutoa wito kwa washiriki walioshindwa kufanya vizuri kwenye mbio hizo kutokata tama bali wajiandae na mashindano yajayo ili waweze kufanya vizuri.

Naye Makamu Mwenyekiti wa mbio hizo Bw Zenno Ngowi alisema mbio hizo zimeweza kufanyika kwa mafaniko makubwa na ushirikiano walioupata kutoka uongozi wa mkoa wa Mwanza na mikoa jirani huku pongezi pia zikielekezwa kwa jeshi la polisi kwa kuhakikisha kila kitu kinaisha kwa usalama .
Chacha Masinde kutoka mkoani Mara akimaliza Rock City Marathon na kuwa mshindi wa kwanza kwenye mbio hizo zilizofanyika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza jana . Chacha alitumia muda wa saa 01:03:00 kumaliza mbio hizo akifuatiwa na mshiriki kutoka nchini Kenya David Kilimo aliyetumia muda wa saa 01:04:40.
Mkuu wa mkoa wa Mwanza Bw John Mongella sambamba na maofisa kutoka benki ya NMB wakishiriki mbio za za km 5.
Washiriki wa mbio za km 21 wakiondoka Uwanja wa CCM Kirumba kuanza safari ndefu.
Ushindani ulikuwa ni mkubwa!


Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...