WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi Maofisa Misitu wanne na kusimamisha shughuli za uvunaji wa mazao ya misitu wilayani Rufiji kwa muda usiojulikana baada ya kutoridhishwa na usimamizi wake.

Maofisa waliosimamishwa kazi ni pamoja na Mkuu wa Idara ya Ardhi, Maliasili na Mazingira Dk. Paul Ligonja, Ofisa Misitu wilaya Gaudens Tarimo, Ofisa Misitu Yonas Nyambuya na Ofisa wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) wa wilaya Seleman Bulenga.

Waziri Mkuu amefanya uamuzi huo leo (Jumatatu, Septemba 26, 2016) wakati akizungumza na watumishi wa wilaya ya Rufiji kwenye ukumbi wa halmashauri kabla ya kuzungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara kwenye viwanya jumba la maendeleo wilayani Rufiji.

Aidha, Waziri Mkuu amemuagiza Mkuu wa Wilaya hiyo, Juma Njwayo kukusanya magogo yoye yaliyoko msituni na kuyapiga mnada na kuitaka  wizara ya Maliasili na Utalii kwenda wilayani Rufiji kufanya uchunguzi wa leseni za uvunaji walizozitoa kwa wilaya hiyo.

Waziri Mkuu amebainisha kwamba wilaya ya Rufiji ni moja kati ya wilaya inayoongoza kwa uvunaji wa mazao ya misitu bila ya kufuata taratibu licha ya kuwa na maofisa misitu.

“Hakuna mafanikio katika sekta ya misitu kwenye wilaya hii ya Rufiji. Nasimamisha shughuli zote za uvunaji wa mazao ya misitu pamoja na watendaji wake kwa sababu hatuwezi kuacha watu wanakata magogo bila ya kufuata taratibu,”

“Haiwezekani Rufiji iwe shamba la bibi, nimesimamisha uvunaji wa magogo hata kwa wenye leseni hadi tuzichunguze zimetoka wapi. Hatuwezi kuruhusu maofisa wanashiriki vitendo vya hujuma kwa kuvuna misitu Rufiji na kugonga mihuli ya Kilwa kisha fedha wanatia mifukoni,” amesema.

Wakati huo huo Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya hiyo Rashid Salum kufuatilia maagizo aliyoyatoa kuhusu kizuizi cha Ikwiriri kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Prof. Jumanne Maghembe alipokutana na watumishi wa wizara hiyo.

Julai 18 mwaka huu Waziri Mkuu alikutana na watumishi wa wizara hiyo jijini Dar es Salaam  na kusisitiza kwamba hakuna sababu ya Serikali kuendelea kuwa na watumishi wasiokuwa na uaminifu, uadilifu na uwajibikaji.

Waziri Mkuu aliitaka wizara hiyo kupunguza idadi ya vizuizi vya ukaguzi wa mazao ya misitu kwenye  barababara  mbalimbali baada ya kukosa tija, alitoa mfano wa barabara ya kwenda mikoa ya kusini  kuanzia Dar es Salaam yenye vizuizi visivyopungua sita na kila kizuizi kinatumika kwa ajili ya kukagua mazao ya misitu na maliasili inayotoka kuvunwa.

Awali mbunge wa Rufiji Mohammed Mchengelwa alilalamikia vitendo vya dharau vinavyofanywa na watumishi wa sekta mbalimbali katika wilaya hiyo jambo linalosababisha wananchi kukosa imani na Serikali yao. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...