Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye akiwapongeza  wachezaji wa Serengeti Boys Jijini Dar es Salaam mara  baada ya  kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Congo-Brazaville iliyofanyika katika Uwanja wa Taifa Septemba 18,2016 Serengeti ilishinda kwa jumla ya goli 3-2.
Na Raymond Mushumbusi - WHUSM. 
 Waziri wa Habari,Utamaduni,Sanaa na Michezo Mhe. Nape Moses Nnauye ameahidi kutoa kiasi cha shilingi Millioni moja kwa kila goli litakalofungwa na Serengeti Boys katika mechi ya marudiano nchini Congo Brazaville. 
 Ametoa ahadi hiyo wakati akiongea na kuwapongeza wachezaji hao mara baada ya kumalizika kwa mchezo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 kati ya Serengeti Boys ya Tanzania na Congo Brazaville uliofanyika katika Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam. 
 “Kwa niaba ya Watanzania wote nawapongeza kwa mchezo mzuri mliouonesha na kuibuka na ushindi lakini bado mnatakiwa kujituma kama mlivyofanya katika mechi hii na naahidi kutekeleza ile ahadi yangu ya laki tano kwa kila goli na nitatoa tena kwenu Millioni moja kwa kila goli mtakalofunga Congo Brazaville.”Alisema Mhe. Waziri Nape.
 Kwa upande wa Kocha wa Timu hiyo Bw. Bakari Shime ameshukuru Waziri na Watanzania kwa ujumla kwa kujitokeza kwa wingi kushuhudia mechi hiyo na watahakikisha wanapata ushindi katika mechi ya marudiano kwani wameshayaona mapungufu yaliyojitokeza na watayafanyia kazi wachezaji watakuwa tayari kuivaa tena Congo Brazavile. 
 Aidha Nahodha wa Timu hiyo Bw. Issa Abdi Makame mbali na kuishukuru Serikali kwa motisha inayotoa ameahidi kujituma zaidi kwa kushirikiana na wenzake na kufuata maagizo kutoka Bechi la ufundi ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo wa marudiano. 
 “Tunashukuru sana kwa motisha mnayotupa na sisi hatutawaangusha tutajituma kadri ya uwezo wetu tupate ushindi tukiwa ugenini ili tuweze kufuzu” Aliongeza Nahodha Makame. 
 Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya umri wa Miaka kumi na saba (Serengeti Boys) inayowania tiketi ya kufuzu kwa fainali za kombe la mataifa ya Afrika (AFCON) kwa vijana yatakayofanyika nchini Madagascar mwaka 2017 inatakiwa kupata ushindi ili kujihakikishia kufuzu kwa fainali hizo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...