THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.


Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

BALOZI WA UINGEREZA NCHINI AMTEMBELEA PROFESA MUHONGO


Na Greyson Mwase, Dar es Salaam

Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke amemtembelea Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo jijini Dar es Salaam lengo likiwa ni kujadili namna Serikali ya Uingereza inavyoweza kufanya kazi na Tanzania kwenye uboreshaji wa sekta za Nishati na Madini.

Balozi Cooke alifanya mazungumzo na Profesa Muhongo pamoja na Watendaji kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA)

Akielezea kuhusu Sekta ya Nishati nchini, Profesa Muhongo alisema kuwa Serikali imeweka mikakati ya matumizi ya vyanzo vya nishati ya umeme kama vile gesi, maji, jotoardhi, makaa ya mawe, upepo, jua na kukaribisha wawekezaji kutoka Uingereza kushirikiana na Serikali kwenye uzalishaji na usambazaji wa umeme nchini hususan katika maeneo ya vijijini.

Aliongeza kuwa, Serikali imeanza kutumia gesi yake iliyogunduliwa kwa wingi kwa kiwango cha futi za ujazo trilioni 57.2 kwa kujenga bomba la gesi kutoka Mtwara hadi jijini Dar es Salaam na kuendelea kusema kuwa Serikali imeweka mkakati wa kusambaza gesi mikoani pamoja na nyingine kuuzwa nje ya nchi.

“Kuna nchi zilizopo Ukanda wa Afrika Mashariki zimeomba bomba la gesi liende kwao; hii itatuwezesha sisi kufanya biashara pamoja nao na kuingiza fedha za kigeni,” alisema Profesa Muhongo

Aliongeza kuwa, mikakati mingine inayofanywa na Serikali ni pamoja na ujenzi wa kiwanda cha kusindika gesi kimiminika ( Liquefied Natural Gas Plant) na kiwanda cha mbolea katika eneo la Kilwa mkoani Lindi na kiwanda kingine cha mbolea katika mkoa wa Mtwara.

Alisisitiza kuwa, bado Serikali inaendelea na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi katika maeneo mbalimbali nchini na kuomba kampuni za Uingereza zenye uzoefu kujitokeza na kuwekeza nchini.
Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (kulia) akielezea fursa za uwekezaji katika Sekta ya Nishati kwa Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke (kushoto). 
Balozi wa Uingereza Nchini, Sarah Cooke akielezea mikakati ya nchi yake katika kuisaidia Tanzania katika uboreshaji wa sekta ya nishati nchini. 
Watendaji kutoka kutoka Wizara ya Nishati na Madini, Shirika la Maendeleo ya Petroli Nchini (TPDC), Shirika la Umeme Nchini (TANESCO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na Wakala wa Ukaguzi wa Madini Nchini (TMAA), wakifuatilia maelezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo (hayupo pichani).