Benny Mwaipaja, MoFP-Washington DC

BENKI ya Dunia inakusudia kuipatia Tanzania ruzuku na mkopo wenye masharti nafuu wa dola Bilioni 1 nukta 6 sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 3 nukta 5 kwaajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo nishati ya umeme, kilimo biashara na ukarabati wa miundombinu ya reli ya kati.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Prof. Benno Ndulu amesema Jijini Washington DC, Marekani ambako Ujumbe wa wataalamu wa masuala ya uchumi na Fedha kutoka Tanzania Bara na Zanzibar wanashiriki mkutano wa mwaka wa Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa IMF kwamba mazungumzo kuhusu mkopo huo yako katika hatua za mwisho.

Prof. Ndulu amesema kuwa upatikanaji wa mkopo huo utaisaidia serikali kuboresha miundombinu yake mbalimbali ili kuharakisha maendeleo ya sekta ya viwanda kwa kuimarisha pia mazingira ya sekta binafsi kufanyabiashara na kuwekeza mitaji na teknolojia.

“Mbali na mkopo huo ambao ni muhimu kwa taifa, tunajadili pia namna ukuaji wa uchumi unavyotakiwa kuakisi maisha ya kawaida ya wananchi wetu kwa kupiga hatua kimaisha na kuondokana na umasikini” alisema Gavana Prof. Ndulu.

Aidha, amesema kuwa Benki ya Dunia imesifu hatua zilizofikiwa na serikali ya Tanzania katika kukuza na kusimamia uchumi wake ambao licha ya uchumi wa dunia kushuka viwango vyake vya ukuaji uliotarajiwa wa asilimia 3.3 na kukua kwa asilimia 1.5 tu, Uchumi wa Tanzania unakua kwa kasi ya asilimia 7.

“Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zinazoendelea ambazo uchumi wake unakua kwa kasi na unatarajia kukua zaidi kutokana na kuvumbuliwa kwa gesi na kushuka kwa mfumuko wa bei” Alisisitiza Prof Ndulu

Kiongozi wa ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa mkopo utakao tolewa ni pamoja na dola milioni mia 2 kwaajili ya kulijengea uwezo shirika la ugavi wa umeme nchini Tanzania-Tanesco ili liondokane na nakisi inayosababishwa na madeni makubwa yanayolikabili shirika hilo

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philiph Mpango akifurahia jambo na Bi. Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi Mkazi anayeiwakilisha Benki ya Dunia katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia wakati wakisubiri kuingia kwenye mkutano Jijini Washington DC.(Picha zote na Wizara ya Fedha na Mipango)
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Dotto James akisalimiana na Bi. Bella Bird ambaye ni Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anaewakilisha benki hiyo katika nchi za Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia akiwa pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Jijini Washington DC.
Bi. Bella Bird, Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia anaewakilisha Tanzania, Burundi, Malawi na Somalia akifafanuliwa masuala mbalimbali ya Tanzania na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Dotto James (kulia) pamoja na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango(katikati) Jijini Washington DC.
Kaimu Kamishna wa Wizara ya Nishati na Madini anayeshughulikia masuala ya Nishati na Petroli Bw. James Andilile akimweleza Kaimu Kamishma wa Sera Bw. Agustine Ollal (kushoto) na Kamishna wa Bajeti Bw. John Cheyo (kulia) kuhusu Tanesco inavyopiga hatua katika uimarishaji wa nishati kwa wananchi, wakati wa Mkutano wa Mwaka wa Benki ya Dunia na IMF unaoendelea Jijini Washington DC, Marekani.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...