Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Abdul-Razaq Badru akizungumza na uongozi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian mjini Bagamoyo jana (Jumanne, Okt 4, 2016). Kushoto kwake ni Mkuu wa Chuo hicho Prof. Peter Msolla.

Na Mwandishi Wetu, Bagamoyo
BODI ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) na Chuo Kikuu cha Kishiriki cha Marian (MARUCO) kilichopo wilayani Bagamoyo mkoani Pwani zimekubaliana kuimarisha ushirikiano kwa kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi.

Akizungumza katika ziara fupi ya kujitambulisha na kubadilishana mawazo chuoni hapo jana (Jumanne, Oktoba 4, 2016), Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru amesema Bodi ya Mikopo inategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wake, vikiwemo vyuo vya elimu ya juu, ili kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yake.

“Tunafanya jitihada za kuongeza ufanisi katika Bodi na ili hili lifanikiwe, tunategemea ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau wetu mkiwemo ninyi waendeshaji wa vyuo vikuu,” amesema Bw. Badru katika mkutano uliohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chuo hicho wakiongozwa na Mkuu wake Prof. Peter Msolla.

Kwa upande wake, Prof. Msolla alimhakikishia Bw. Badru na Serikali kwa ujumla kuwa chuo chake kitaendelea kuimarisha ushirikiano uliopo kati ya Bodi na Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian kwa kutekeleza wajibu wake kwa wakati na ufanisi.

Awali akiongea katika mkutano huo, Prof. Msolla alisema chuo hicho kilipata usajili kutoka Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) mwezi Aprili mwaka jana (2015) na kuzinduliwa na Rais Mstaafu Dkt. Jakaya Kikwete mwezi Mei mwaka jana (2015) na kupokea wanafunzi 421 katika mwaka wake wa kwanza wa masomo. 

Kwa mujibu wa Prof. Msolla, chuo hicho kimejikita katika ufundishaji wa kozi tatu za masomo ya sayansi na hisabati ambayo wataalamu wake wanahitajika sana nchini kote. Kozi hizo ni pamoja na Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Ualimu (BSc. Edu), Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Ualimu wa Hisabati na Takwimu (BSc. Maths & Statistics); na Shahada ya Kwanza ya Sayansi ya Kompyuta (BSc. Computer).

Chuo Kikuu Kishiriki cha Marian (MARUCO), ambacho ni sehemu ya Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino(SAUT), kinatarajia kuanza mwaka huu (2016/2017) wa masomo tarehe 17 Oktoba, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...