Wafanyakazi wa Benki ya CRDB na viongozi na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Mbulu wakifurahia jambo baada ya benki hiyo kukabidhi madawati 200 katika wiki ya huduma kwa wateja, kupitia kauli mbiu ya tunakusikiliza karibu tukuhudumie.
Wafanyakazi wa benki ya CRDB na wanafunzi wa shule ya Imboru ya Halmashauri ya Mji wa Mbulu Mkoani Manyara, wakishangilia baada ya benki hiyo kukabidhi madawati 200 kwenye halmashauri hiyo.
HALMASHAURI ya Mji wa Mbulu Mkoani Manyara, imekabidhiwa msaada wa madawati 200 na Benki ya CRDB kwa ajili ya kutumiwa na wanafunzi wa shule tano za msingi, ambapo kila shule itapatiwa madawati 40.

Meneja wa CRDB Tawi la Babati, Ronald Paul akizungumza wakati wa kukabidhi madawati hayo 200 alisema katika kuadhimisha wiki ya huduma kwa wateja wamejitolea msaada huo kama mchango wao kwa jamii.

Paul alisema benki hiyo ya CRDB imetoa madawati hayo 200 ambayo yatagawanywa kwa wanafunzi wa shule tano za halmashauri ya mji wa Mbulu, ambapo kila moja ya shule hizo zitatolewa madawati 40.

“Tukiwa kwenye wiki ya huduma kwa wateja tunahakikisha tunarudisha kile kidogo tunachopata kupitia jamii, sisi tutaendelea kutoa mchango wetu kwa jamii ili kuhakikisha tunaunga mkono suala zima la maendeleo,” alisema Paul.

Alisema kwa muda wa miaka miwili tangu CRDB ianze kutoa huduma zake katika mkoa wa Manyara, wananchi wa mji wa Mbulu wamechangamkia fursa ya uwepo wao, kwa kuweka fedha, kutoa na kuchukua mikopo ya benki hiyo.

Mkurugenzi wa mji wa Mbulu Anna Mbogo akizungumza wakati akipokea madawati hayo aliushukuru uongozi wa CRDB kwa kutoa msaada huo kwani utawasaidia wanafunzi wa shule hizo kusoma kwa ufasaha.

Mbogo alisema awali walikuwa na upungufu wa madawati 3,179 ila walijitahidi na kuhakikisha madawati hayo yanapatikana na hadi sasa wana madawati 999 ya ziada ambayo yamehifadhiwa kwa ajili ya kutumika baadaye.

Alitoa ombi kwa CRDB kuendelea kutoa msaada wa miundombinu ya shule za eneo hilo kwani hivi sasa wana mpango wa kujenga madarasa mengine ya shule ya msingi Imboru, yenye madarasa mawili pekee.

“Awali wanafunzi wa shule hii walikuwa wanatembea umbali mrefu wa kilometa tatu kutoka nyumbani hadi shuleni kila siku hivyo ili kukomesha hali hiyo kwa watoto hawa wadogo ndipo tukaamua kuijenga,” alisema Mbogo.

Alisema lengo lao ni kuhakikisha wanaendelea kuiboresha shule hiyo mpya kwa kujenga madarasa mengine zaidi ili baada kwani hivi sasa wanafunzi hao wanapata elimu kwa urahisi kwa sababu ipo karibu na makazi yao.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...