THIS BLOG IS PROUDLY SPONSORED BY VODACOM, TANZANIA'S LEADING CELLULAR NETWORK. | CRDB BANK - THE BANK THAT LISTENS | NATIONAL BANK OF COMMERCE (NBC)- CONVENIENTLY EVERYWHERE | NATIONAL SOCIAL SECURITY FUND (NSSF) | PUBLIC SERVISE PENSIONS FUND (PSPF). ' Karibu katika hii Globu ya jamii. Una karibishwa kutoa maoni yako yoyote yatakayo jenga taifa letu. Nawasihi kila mmoja wetu ajiheshimu kwa kutumia lugha zisizochafua hali ya hewa. Yaliyomo humu hayahusiani kwa vyovyote vile na hariri za magazeti ya Daily News, HabariLeo na Sunday News. Maoni yanayotolewa na wasomaji si ya GLOBU YA JAMII, ni ya mtoa maoni isipokuwa pale itavyoelezwa vinginevyo. Akhsanteni sana na tuendeleze Libeneke.

Gadget

This content isn't available over encrypted connections yet.

MKURUGENZI WA HABARI AWATAKA WADAU WA TASNIA YA HABARI KUTOA MAONI KUHUSU MUSWADA WA HABARI

Na Beatrice Lyimo.

SERIKALI imevitaka wadau wa vyombo vya habari nchini kuacha kulalamika na badala yake waendelee kutoa maoni yao kuhusu muswada wa sheria kwa vyombo vya habari ambao unatarajiwa kuwasilishwaa katika Bunge lijalo mjini Dodoma.

Akizungumza katika wakati tofauti wakati wa ziara yake ya kutembelea Taasisi za Vyombo vya habari nchini, Mkurugenzi wa Idara ya Habari(MAELEZO), Hassan Abbas alisema lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa muswada huo unapitishwa na Bunge ili uweze kuwa sheria kamili na hatimaye kuifanya tansia ya habari kuzidi kuheshimika.

Mkurugenzi Abbas alisema tangu muswada huo uliposomwa kwa mara ya kwanza Bungeni, mwezi Septemba mwaka huu, wadau wa tasnia ya habari nchini ikiwemo Wahariri na waandishi wa habari wamekuwa mstari wa mbele kupingana katika mitandao ya kijamii badala ya kutoa maoni yao katika mamlaka zinazohusika.

“Ni aibu kwa maoni ya muswada huu yanayohusu tasnia ya habari kutolewa na watu ambao hawana taaluma ya habari, hivyo tukiwa kama wanataaluma ni vyema tujitokeze kwa wingi kutoa maoni kifungu kwa kifungu ili kuweza kuboresha muswada” alisema Mkurugenzi Abbas.

Aliongeza kuwa haitopendeza kwa muswada huo kuendelea kutolewa maoni na wananchi wengine na wadau wa muswada kukacha kutoa maoni yao, na hivyo kusababisha muswada huo kuandikwa na watu walio nje ya tasnia ya habari.

Abbas alisema, muswada huo utakusudia kuiongezea nguvu tasnia ya habari kwa kuweka ikiwemo suala zima la kuzingatia sheria na mipaka ya nchi katika utoaji wa habari na taarifa maalum za Serikali kwa umma kwa kuzingatia ukomo wa kimataifa.

“Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948, pamoja na kuzungumzia kuhusu haki ya kupata taarifa lakini pia limeanisha sheria mbalimbali ambazo hazina budi kuheshimiwa, na sheria hizo ni pamoja na sheria za ulinzi na usalama” alifafanua Mkurugenzi Abbas.

Akifafanua zaidi alisema taaluma ya habari ni tasnia muhimu katika maendeleo ya taifa ila kwa upande mwingine inaweza kuharibu maendeleo kwa njia moja au nyingine na hivyo kuwataka wadau wa habari kujitokeza kutoa maoni kwa kujenga hoja za msingi ili kuboresha muswada badala ya kulalamika.

Aidha kwa upande mwingine, Abbas alisema Ofisi yake ni mlezi na mratibu wa vyombo vya habari na hawana budi kuwasiliana naye pindi wanapopata changamoto mbalimbali ikiwemo utoaji na upatikanaji wa taarifa za Serikali katika Wizara, Taasisi, Idara, Mikoa na halmashauri nchini.

Pia alisema zipo taarifa ambazo zinahitaji kufanyiwa uhakiki ikiwemo ufundi na takwimu, na hivyo aliwataka waandishi wa habari kuwa wavumilivu pale wanapohitaji taarifa hizo kutoka kwa maafisa habari wa Wizara au Taasisi husika.

Kwa upande wake, Mhariri Mtendaji wa gazeti la Majira, Imma Mbughuni alisema chombo hicho kimejipanga kutoa maoni yao kuhusu muswada huo na mara baada ya kumaliza wanatarajia kuwasilisha katika kamati ya kudumu ya Bunge.

Naye Mhariri Mtendaji wa Gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa alisema chombo chao pia kimekusudia kuupitia muswada huo ili kutoa maoni yao na baadae kuyawasilisha katika kamati husika.
Mkurugenzi wa Habari, Hassani Abbas (kulia) akizungumza jambo na Mwandishi Mwadamizi wa Gazeti la Jambo Leo, Mashaka Mgeta (kushoto) wakati wa ziara ya kutembelea ofisi za gazeti hilo pamoja na kubadilisha uzoefu wa kazi leo Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Mhariri Mtendaji Anicetus Mwesa.

Mkurugenzi wa Habari, Hassani Abbas (kushoto), akizungumza na Wahariri Waandamizi wa Gazeti la Jambo Leo, Anicetus Mwesa (katikati), Exuper Kachenje na Kizito Noya wakati wa ziara ya kutembelea ofisi za gazeti hilo pamoja na kubadilisha uzoefu wa kazi leo Jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Habari, Hassani Abbas (kushoto), akizungumza na Wahariri Waandamizi wa Gazeti la Jambo Leo, Joseph Lugendo (kushoto), na Joseph Kulngwa wakati wa ziara ya kutembelea ofisi za gazeti pamoja na kubadilisha uzoefu wa kazi leo Jijini Dar es Salaam.