Na Mahmoud Ahmad Arusha.
MAHAKAMA ya hakimu mkazi Arusha imemwachia huru mwanafunzi wa mwaka wa tatu katika chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru(CDTI),Allan Mbando baada ya kumwona hana hatia katika kesi ya tuhuma za kufanya uchochezi kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.

Mbando,alikamatwa hivi karibuni na jeshi la polisi mkoani Arusha na kisha kufikishwa mbele ya mahakama hiyo kwa kosa la kusambaza ujumbe kupitia Facebook uliosema kuwa”Mwamunyange pindua nchi haiwezekani wote wawe nje ,halafu hakuna aliyepewa mamlaka ya kukalia kile kiti”.

Akitoa hukumu hiyo jana hakimu mkazi wa mahakama hiyo,Augustine Rwizile alisema kuwa mahakama imemwachia huru mtuhumiwa huyo baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha shtaka dhidi yake pasipo kuacha shaka yoyote.

Hakimu alisema licha ya kumwachia huru,upande ambao haujaridhika unaweza kukata rufaa.

Mbele ya pande zote hakimu huyo alisema kwamba mahakama imemwachia huru mtuhumiwa huyo kwa kuwa ushahidi uliowasilishwa na upande wa jamhuri hautoshi kumtia hatiani mtuhumiwa huyo na pia hakuna jambo lolote lenye nia ovu katika ujumbe uliosambazwa na mtuhumiwa kwa lengo la kufanya uchochezi.

Hakimu Rwizile alisema kwamba ujumbe uliosambazwa na mtuhumiwa huo haukuwa na umuhimu wowote kwa kuwa haujaelezea Mwamunyange ni nani lakini pia haujataja nchi husika ambayo ililengwa kupinduliwa.

Hakimu huyo aliiambia mahakama hiyo ya kwamba mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa akiwakilishwa na wakili wa kujitegemea mkoani hapa ,Moses Mahuna ameachiwa huru na mahakama hiyo kwa kuwa ushahidi uliowasilishwa mbele ya mahakama hauthibitishi ujumbe uliosambazwa mitandaoni ulitoka kwa mtuhumiwa huyo.

“Kwanza ujumbe hauonyeshi ni nani huyo Mwamunyange,pili haujataja nchi inayodaiwa kutaka kupinduliwa lakini tatu ujumbe hauonyeshi jambo lolote la msingi lenye mahusiano ya kisiasa katika taifa linalodaiwa kupotoshwa”alisema hakimu huyo.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...