Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila
Kabange ameweka jiwe la msingi la jengo la Kituo cha Pamoja cha Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ambalo limejengwa kwa lengo la kuwaweka
pamoja wadau wote wanaotoa huduma katika bandari ya Dar es Salaam ikiwa ni
juhudi za kuboresha huduma na kupunguza gharama kwa watumiaji wa bandari hiyo.
Hafla ya uwekaji jiwe la msingi la jengo hilo refu kuliko
yote Afrika Mashariki na kati imefanyika leo tarehe 04 Oktoba, 2016 na
kushuhudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli.
Akizungumza kabla ya kuwekwa jiwe hilo la msingi Rais Magufuli
ameishukuru Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa kuwa mteja mkubwa wa bandari
ya Dar es Salaam na amesema aliamua jiwe la msingi la jengo hilo liwekwe na
Rais wa Kongo kwa kutambua umuhimu wa nchi yake katika biashara ya bandari ya
Dar es Salaam na pia undugu na urafiki wa kihistoria uliopo kati ya nchi hizi
mbili.
Rais Magufuli amemhakikishia Rais Kabila kuwa kama ambavyo
Serikali yake imechukua hatua kadhaa za kurekebisha kasoro zilizokuwepo katika
bandari hiyo, itaendelea kujenga mazingira mazuri zaidi kwa wafanyabiashara wa
Kongo kutumia bandari hiyo ikiwa ni pamoja na kudhibiti vitendo vya rushwa,
kuongeza muda wa kutunza mizigo inayoshushwa kutoka siku 14 hadi siku 30,
kuanzisha bandari kavu katika eneo la Ruvu mkoani Pwani na kuinua ari ya
wafanyakazi wa bandari kutoa huduma bora.
"Mhe. Rais Kabila bandari yetu ilifikia mahali pa
kuandika rekodi ya kupotea kwa meli kwenye taarifa za bandari, kuna wakati hapa
zilipotea meli 60, lakini pia mizigo ya watu ilikuwa inapotea na
wafanyabiashara walikuwa wanaombwa rushwa.
"Kuna baadhi ya wafanyakazi wa bandari waliifanya hii
bandari kama mali yao, walikuwa wanaondoka na fedha za rushwa kwenye buti za
magari, naomba nikuhakikishie kuwa haya hayatatokea tena, na yakitokea Mhe.
Balozi wa Kongo upo hapa njoo unieleze mimi au mwambie Makamu wa Rais au Waziri
Mkuu"
amesisitiza Rais Magufuli.
Dkt. Magufuli pia amempongeza Rais Mstaafu wa awamu ya nne
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete kwa kuanzisha ujenzi wa jengo hilo la Mamlaka ya
Usimamizi wa Bandari Tanzania na kwamba anaamini litasaidia kuimarisha biashara
kati ya Tanzania na Kongo na nchi nyingine zinazotumia bandari ya Dar es
Salaam.
Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Mhe. Joseph Kabila Kabange amemshukuru Rais Magufuli kwa heshimu kubwa aliyompa
yeye na nchi ya Kongo ya kuweka jiwe la msingi la jengo hilo na amesema
kutokana na Tanzania kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za bandari
ya Dar es Salaam mizigo ya Kongo itapitia bandari hiyo.
"Mhe. Rais Magufuli bandari hii ipo Dar es Salaam
lakini bandari hii ni ya kwetu sote, mashariki ya Kongo inapakana na nchi nne
za Tanzania, Rwanda, Burundi na Uganda lakini asilimia 50 ya mizigo inatoka
Tanzania hususani katika bandari ya Dar es Salaam.
"Nimefurahi pia kuwa katika juhudi za Tanzania
kuboresha bandari pia mnaboresha barabara na bandari ndogo ndogo za ziwa
Tanganyika, hili ni jambo muhimu kwa sababu sasa mizigo ya Kongo itasafiri kwa
urahisi na wafanyabishara wa Kongo waliokuwa wameacha kutumia bandari ya Dar es
Salaam watarudi"
amesema Rais Kabila.
Mhe. Joseph Kabila Kabange amesema katika miaka ya 70 na 80
Kongo ilikuwa ikizalisha shaba kiasi cha tani laki 1 lakini hivi sasa
inazalisha hadi tani Milioni 1.2 na zote hizi zinategemewa kusafirishwa nje ya
nchi kupitia bandari ya Dar es Salaam.
Ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kununua ndege mbili
aina ya Bombardier Q400 na ameunga mkono mpango wa kuanzisha safari za moja kwa
moja kati ya Tanzania na Kongo huku akibainisha kuwa nchi yake pia itanunua
ndege kwa ajili ya kuimarisha zaidi usafiri wa anga kati ya nchi hizi mbili.
Mapema kabla ya Marais wote wawili kuzungumza, Mkurugenzi
Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Deodatus Kakoko
alisema jengo hilo lina ghorofa 35, urefu wa meta 157, ukubwa wa meta za mraba
65,115 na ujenzi wake unatarajiwa kukamilika tarehe 31 Desemba, 2016 kwa
gharama ya Shilingi Bilioni 130.
Rais Kabila ambaye aliingia hapa nchini jana tarehe 03
Oktoba, 2016 kwa ziara ya kiserikali ya siku tatu, jioni ya leo atahudhuria
dhifa ya kitaifa katika ukumbi wa Ikulu Jijini Dar es Salaam iliyoandaliwa kwa
ajili yake na Mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John
Pombe Magufuli.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
04 Oktoba, 2016
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akimshuhudia mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila akifunua pazia kuashiria kuwekwa kwa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.PICHA NA IKULU.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli akihutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila akihutubia katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila akipokea zawadi ya picha ya Bandari ya Dar es salaam kutoka kwa mwenyekiti wa Bodi ya TPA Bw. Ignas Aloys Rubaratuka katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la Jengo la ONE STOP CENTRE la Mamlaka ya bandari (TPA) jijini Dar es salaam leo Oktoba 4, 2016.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkr John Pombe Magufuli na mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) Mhe. Joseph Kabila katika sherehe za uwekaji wa jiwe la msingi la wakipata maelezo toka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mhandisi Deusdedit Kakoko.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...