Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila akipunga mkono wakati akipanda ndege kurejea nchini kwake mara baada ya kumaliza ziara yake ya siku tatu hapa nchini 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akiwa pamoja na  Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan wakipunga mkono kuagana na Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila (hayupo pichani) katika Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA).
  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akisalimiana na Shekhe Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Alhadi Mussa Salum katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere mara baada ya kuagana na mgeni wake Rais wa wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Joseph Kabila. kulia ni mkuu wa Wilaya ya Ilala Sofia Mjema.
PICHA NA IKULU.

RAIS wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Mhe. Joseph Kabila Kabange leo tarehe 05 Oktoba, 2016 amemaliza ziara yake ya kiserikali ya siku tatu hapa nchini na kurejea nchini kwake.

Katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam Rais Kabila ameagwa na mwenyeji wake Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.

Viongozi wengine walioungana na Rais Magufuli wakati wa kumuaga Rais Kabila ni Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, Mawaziri, Mabalozi wa nchi mbalimbali, Wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Paul Makonda na Viongozi wa Dini.

Katika hatua nyingine, mara baada ya kuondoka kwa Rais Kabila, Rais Magufuli amefanya ukaguzi wa kushitukiza katika sehemu ya kukagulia mizigo na abiria ya uwanja huo upande wa Terminal One ambako Mwezi Mei mwaka huu alitembelea kwa kushitukiza na kubaini kuwa mashine za ukaguzi (Scanners) zilikuwa hazifanyi kazi.

Mara hii Rais Magufuli amebaini kuwa mashine hizo zinafanya kazi, baada ya kujionea yeye mwenyewe uhalisia wa namna mizigo inavyokaguliwa.

Hata hivyo amemuagiza Mkurugenzi wa uwanja wa ndege wa Julius Nyerere Bw. Paul Rwegasha kuwachukulia hatua za kinidhamu maafisa wawili  walitoa taarifa za uongo pindi alipofanya ukaguzi wa kushitukiza mara ya kwanza.
"Leo kweli mashine zinafanya kazi na mimi nimeona lakini wale walionidanganya mara ya kwanza nilipokuja, Mkurugenzi hakikisha unawachukulia hatua" amesisitiza Dkt. Magufuli.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
05 Oktoba, 2016.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Duh huo mdege wa Congo !kama tule tundege twetu tuwili twapya!!

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...