Na A.O. Ali
Kampuni mashuhuri ya
filamu ya Banyak kutoka nchini Uingereza, imetangaza nia na dhamira yake ya
kufanya kazi pamoja na kampuni ya Rafiki Network nchini Tanzania katika kufanikisha tukio lake
la kwanza la resi ndefu za ngalawa litakalofanyika tarehe 18 Disemba, 2016,
huko Vumawimbi kisiwani Pemba visiwani Zanzibar.
Akitoa taarifa huyo kwa mwandishi wa habari hii kupitia mazungumzo
ya simu, Rais wa kampuni ya Rafiki Network Bwana Hamad Omar Hamad amethibitisha
kuwa mazungumzo kati yao na kampuni ya Banyak yameshakamilika na kwa sasa
kampuni hiyo inakamilisha utaratibu wa kujiandaa kwa ajili ya tukio hilo.
“ Napenda niwahakikishie kuwa baada ya kuliona wazo letu hili la
kutaka kuanzisha resi ndefu za ngalawa
hapa Afrika Mashariki, wenzetu wa BANYAK wa kule Uingereza hawakufikiri mara
mbili. Wamesema wako tayari kuja nchini kushirikiana nasi kikamilifu.” Alisema Bwana Hamad.
Aidha Bwana Hamad amesema amefarijika sana kuwa licha ya kuwasiliana
na wadau wengi wa biashara yakiwamo mashirika ya simu, ndege na usafiri wa
baharini, imempa moyo sana kuona kwamba kampuni hii ya kigeni ndiyo imekuwa ya
kwanza kuona fursa adhimu na kujitokeza kushiriki katika tukio hili adhimu na
la kihistoria nchini.
“ Wenzetu wa Banyak hawakujali tukio hili linaandaliwa na nani, wapi
na vipi. Baada ya kuona baadhi ya maandiko na posta ya tangazo la tukio letu, imewatosha
wao kuona kuwa kuna fursa kubwa katika tukio hili. Kwa kutambua umhimu wa tukio
lenyewe wameamua kuchukua gharama na muda wao kuja kushiriki kikamilifu katika
kufanikisha tukio letu hili. Kwa kweli ni habari njema sana kwetu!” Alisema Bwana
Hamad.
Kampuni ya Banyak ni moja kati ya kampuni mashuhuri nchini Uingereza
ambayo kwa muda mrefu imekuwa ikijishughulisha na kuandaa makala za video
(documentary) zenye kuelimisha jamii.
Kampuni hiyo yenye makazi yake jijini London, itaingia makubaliano ya kurikodi
tukio zima la resi za ngalawa zitakazofanika Pemba mwishoni mwa mwaka huu. Resi
hizo ndefu zaidi kuwahi kutokea katika pwani ya Afrika Mashariki zitaanzia
bandari ya Vuma wimbi na kuishia bandari ya Tumbe, takribani mwendo wa kilomita
30 za baharini.
Resi hizo zitashirikisha Ngalawa kutoka maeneo mbali mbali ya
Tanzania sambamba na kuwashirikishi kikamilifu wamiliki wa ngalawa kutoka
maeneo enyeji ya Tumbe, Shumba mjini, Kiuyu, Msuka, Tondooni na kwengineko
ambapo ngalawa kati ya 30 hadi 50 zitashiriki.
Kampuni ya Rafiki Network imeanzishwa mwaka 2016 na kusajiliwa
visiwani Zanzibar ambapo miongoni mwa kazi zake ni kuandaa matukio mbali mbai
ya Elimu na Utamaduni kwa lengo la kuiwezesha jamii kimaisha kwa kufungua
milango ya fursa za ajira sambamba na kukuza utalii wa ndani na wa nje hapa
nchini.
Resi hizi za Ngalawa ndio tukio la mwanzo kubwa kuandliwa na Kampuni
ya Rafiki Network ambapo wadau mbali mbali kama ZANTEL, TIGO, HALOTEL, ZSSF,
Vigor Group of Companies, TASAKHTA Hospitals na Sun Tours zimeombwa kudhamini
tukio hili. Kampuni nyengine ni Hotel ya Tembo, Serena na nyenginezo ambapo pia
mashirika mbali mbali ya ndege pia yameombwa
kutoa udhamini.
“ Kwa hakika tuna tamaa kubwa ya kupata mashirikiano na wadhamini
wetu. Hadi sasa TASAKHTA Hospital na Sun Tours wamejitokeza rasmi kudhamini
sehemu ya tukio hili. Hata hivyo tunawakaribisha wadhamini wengine waweze
kuiona fursa iliyopo mbele yao na wajitokeze kudhamini tukio hili lenye manufaa
kwao na jamii kwa ujumla.” Bwana Hamad Omar alitoa wito sambamba na kuushukuru
Uongozi wa Hospitali ya TASAKHTA na Kapmuni nguli ya utalii visiwani Zanzibar
ya SUN Tours kwa kukubali kushiriki na kudhamini sehemu ya tukio hili.
Tukio hili sambamba na kudhaminiwa na mashirika mbali mbali
linatarajiwa kuhudhuriwa na vyombo mbali mbali vya habari vya ndani na nje ya
nchi ambapo idadi kubwa ya wageni na washabiki inatarajiwa pia kujitokeza kwa
wingi kujionea tukio hili la kihistoria katika nchi yetu.
Toa Maoni Yako:
0 comments so far,add yours
Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...