Serikali imesema itaongeza mabehewa ya abiria na mizigo katika Shirika la Reli la Tanzania (TRL), kwa lengo la kutatua adha ya usafirishaji kwa watumiaji wa reli ya kati katika mikoa ya Tabora, Kigoma na Katavi.

Akizungumza katika ziara yake ya kikazi mkoani Tabora, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa uhaba wa mabehewa ya abiria umesababisha wananchi wa maeneo hayo kutumia njia zisizo rasmi za ununuzi wa tiketi kwa ajili ya usafiri huo.

“Serikali imetambua changamoto kubwa ya usafiri inayowakabili wakazi wa mikoa hii, hivyo ni wakati muafaka kwa TRL kuongeza mabehewa matatu ili kupunguza adha ya usafiri”, amesema Prof. Mbarawa

Aidha, Waziri Prof. Mbarawa ameupongeza uongozi wa TRL kwa kuokoa matumizi ya zaidi ya Shilingi milioni 100 kwa kukarabati mabehewa ya mizigo 23 kwa kutumia wataalam wazawa wa shirika hilo.

Ameongeza kuwa Shirika hilo limetekeleza dhana ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kupunguza matumizi ya fedha na kuzingatia thamani ya fedha na kazi inayofanyika.

“Nawapongeza kwa kazi nzuri mnayofanya ya kupunguza matumizi ya fedha mnazopata kwenye Shirika, ninaomba muendelee kutumia vyanzo vya ndani ili shirika lifikie hatua ya kujitegemea” amesema Profesa Mbarawa.

Naye, Meneja wa Usafirishaji wa TRL, mkoa wa Tabora Fredrick Masangwa ameiomba Serikali kuendelea na maboresho katika miundombinu ya reli kwa kiwango sawa na jinsi inavyoboresha miundombinu shindani ya barabara ili kuwepo na ushindani sawa katika sekta hizo mbili za usafirishaji.

Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa amekagua ujenzi wa barabara ya Ndono-Urambo kwa kiwango cha lami yenye urefu wa KM 52 na barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 na kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi na ukarabati wake.

Profesa Mbarawa amesema kuwa ujenzi wa miradi hiyo iende sambamba na viwango bora vya ujenzi wa barabara vilivyomo kwenye mikataba iliyosainiwa.


Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na mkandarasi wa Kampuni ya China Civil pamoja na viongozi wa Serikali mkoani Tabora wakati akikagua ujenzi wa barabara ya Ndono-Urambo yenye urefu wa KM 52 kuona hatua iliyofikiwa. . 
Mkandarasi wa Kampuni ya Chicco kutoka China (kushoto), akitoa taarifa ya ujenzi wa barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 kwa Waziri wa Ujenzi Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kulia), alipokagua barabara hiyo kuona maendeleo yake. 
Mbunge wa Jimbo la Kaliua mkoani Tabora, Mhe. Magdalena Sakaya akifafanua jambo kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa wakati alipokagua barabara ya Kaliua-Kazilambwa yenye urefu wa KM 56 kuona maendeleo yake. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...