Na Jacquiline Mrisho - MAELEZO

Serikali ya awamu ya tano imejipanga kukuza ujuzi wa nguvu kazi kwa vijana takribani 15,000 kwa mwaka wa fedha 2016/2017 ili kuwaongezea uzoefu wa kazi na kuongeza fursa za upatikanaji wa ajira.

Ujuzi wa nguvu kazi nchini utatolewa kupitia programu maalum ya mafunzo kazini kwa njia ya Uanagenzi (Apprenticeship), mafunzo kwa vitendo  kwa wahitimu (Internships) pamoja na urasimishaji  wa ujuzi uliopatikana kwa mfumo usio rasmi (Recognition of Prior Learning).

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi wa Ajira, Ally Msacky alipokuwa akimuwakilisha Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde wakati wa mahafali ya mwisho ya vijana waishio katika mazingira magumu waliohitimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Future World.

Mhe. Mavunde amesema kuwa maendeleo ya nchi yoyote yanategemea nguvu kazi ambayo kwa asilimia kubwa inatoka kwa vijana kwahiyo ni wajibu wa kila mmoja kuhakikisha vijana wanapatiwa elimu na mafunzo ili waweze kujiajiri au kuajiriwa na hatimaye kupunguza utegemezi na kuongeza pato la Taifa.

“Napenda nitumie fursa hii kuwataarifu kuwa Serikali yetu imetoa kipaumbele cha juu katika kujenga ujuzi wa nguvu kazi, takribani vijana 15,000 watafaidika na programu hiyo kwa mwaka huu wa fedha kwani tayari tumeanza kutekeleza kwa kuingia mikataba na Makampuni ya kutoa mafunzo kwa vitendo katika maeneo ya kazi”, alisema Mhe. Mavunde.

Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kusimamia Sera ya Taifa ya Ajira na Sera ya Elimu ya Mafunzo ya Ufundi Stadi kwa lengo la kuweka msisitizo katika kuweka mazingira na kutoa elimu ya ufundi stadi kwa ngazi mbalimbali ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira na hatimaye kuongeza fursa za ajira nchini.

Aidha Mhe. Mavunde amehaidi kuendelea kushirikiana na Taasisi mbalimbali za ndani na nje ya nchi ili kuhakikisha kuwa ukuzaji wa ajira kwa vijana unapewa kipaumbele pia ameahidi kusaidia kuimarisha utekelezaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao unawasaidia vijana kupata mikopo kwa masharti nafuu.


Mradi huu wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi - Dar es Salaam (DYEE) kupitia mafunzo ya stadi za kujiajiri (BEST Model) unafadhiliwa na Benki ya NBC na kuratibiwa na Shirika la Plan International, umetekelezwa katika kipindi cha miaka 3 na umetoa mafunzo kwa jumla ya vijana 1,225.


Mkurugenzi wa Ajira, Ally Msacky akisoma hotuba ya Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Mhe. Anthony Mavunde alipoenda kumuwakilisha katika mahafali ya mwisho ya vijana waliopo chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi – Dar es Salaaam (DYEE) waliohitimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Future World, kushoto ni Muwakilishi wa Mkurugenzi Mkazi wa Plan International – Tanzania, Bi. Gwynneth Wong na kulia ni Mkuu wa Chuo hicho, Robert Mkolla. Mradi huo umefadhiliwa na Benki ya NBC na kuratibiwa na Shirika la Plan International.  


Mmoja wa vijana waliopo chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi – Dar es Salaaam (DYEE) waliohitimu katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi cha Future World, Hamis Abdallah akimuonyesha Mkurugenzi wa Ajira - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Ally Msacky jinsi ya kuchanganya vinywaji na kupata kinywaji kimoja (cocktail) katika siku ya mahafali yao. Mradi huo umefadhiliwa na Benki ya NBC na kuratibiwa na Shirika la Plan International.

 Mkurugenzi wa Ajira - Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Ally Msacky akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya vijana waliohitimu mafunzo ya ufundi katika Chuo cha Future World chini ya mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi – Dar es Salaaam (DYEE). Mradi huo umefadhiliwa na Benki ya NBC na kuratibiwa na Shirika la Plan International.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

Kuna Maoni 1 mpaka sasa

  1. Recognition of prior laerning inakuja. Hii ni neema ndugu zanguni na itapunguza wale wanao-forge vyeti. Tujitume twende mbele ki-mmoja mmjoa na nchi yetu kwa ujumla. HAbari njeme hizi. Alhamdulilah

    ReplyDelete

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...