Na Jacquiline Mrisho – MAELEZO, Dodoma.

Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii, Peter Serukamba amesema kuwa sheria ya Huduma za Habari itatungwa kulingana na maoni yaliyowasilishwa kutoka kwa baadhi ya wadau ili muswada huo usihairishwe kama miaka iliyopita.

Hayo yamesemwa leo Mjini Dodoma na Mwenyekiti ya Kamati hiyo alipokuwa akiongea na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya kamati hiyo baada ya kuongeza muda wa siku 10 kwa wadau ili waweze kuusoma kwa makini muswada huo.

Serukamba amefafanua kuwa Muswada ukishasomwa kwa mara ya kwanza ni jukumu la wananchi kutoa maoni yao juu ya suala husika lakini kwa miaka takribani 23 wadau wa tasnia ya habari hawajaonesha nia ya utayari wa kutoa maoni yao na kuendelea kuiomba Serikali kuupeleka mbele mswada huo.

“Kwa mwaka huu tena wadau hawa waliomba Muswada huu usogezwe mbele, lakini hatuwezi kuacha kutunga sheria kila siku kwa sababu ya baadhi ya wadau kutoleta maoni yao, tutaendelea kutunga sheria hii kulingana na maoni yaliyowasilishwa na baadhi ya wananchi na wadau”, alisema Serukamba.

Amesema kuwa tangu mwaka 1993 huu ndiyo umekuwa mchezo unaofanywa na wadau wa tasnia hiyo ambapo kwa mwaka huu pia wadau hao walikuja na maoni lakini kwa makusudi waliamua kutoyatoa.

Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa Oktoba 31 mwaka huu watakutana na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Nape Nnauye kwa ajili ya kukubaliana juu ya vifungu ambavyo wamekuwa wakivijadili kwenye vikao vya kamati ili kuviweka kwenye Muswada tayari kwa kwenda kusomwa Bungeni.

Aidha, amewataja baadhi ya wadau wa tasnia hiyo ambao wamekiri kupokea barua ya mwaliko wakuhudhuria kikao cha kamati hiyo kuwa ni Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Pili Mtambalike, Umoja wa Vyama vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) na Baraza la Habari Tanzania (MCT).

Amewashukuru wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa habari waliotoa maoni yao na amewatoa hofu kuwa muswada huo utatendewa haki na itatungwa sheria nzuri ambayo itarudisha heshima ya tasnia hiyo.

Muswada huo ulisomwa bungeni kwa mara ya kwanza Septemba 16 mwaka huu na Waziri mwenye dhamana Mhe. Nape Nnauye ambapo baada ya hapo wananchi walitakiwa kuusoma na kutoa maoni yao.
Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii wakiendelea na kazi ya kuchambua maoni yaliyotumwa na wadau wa habari ili kuboresha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari leo mjini Dodoma.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...