Shirikisho la Michezo ya Wizara na Idara za Serikali (SHIMIWI) katika Kalenda ya mwaka 2016 ilipanga michezo ya SHIMIWI ifanyike mkoani Dodoma kuanzia tarehe 14-27 Novemba, 2016.

Kama mnavyofahamu hivi karibuni Taifa limekumbwa na janga la tetemeko la ardhi Mkoani Kagera.  Janga ambalo limesababisha vifo, limeacha familia nyingi kukosa makazi.  Tetemeko hili limeleta madhara makubwa. Taasisi, Mashirika, nchi mbalimbali na watu binafsi wameguswa kwa ajili ya kuchangia waathirika wa tetemeko ili kukabiliana na madhara yaliyotokea.

Katika kutimiza dhamira ya kuleta maendeleo katika Taifa Serikali  ya awamu ya tano imeendelea kuchukua hatua mbalimbali ili kuleta ufanisi.  Zikiwemo kuahirisha Maadhimisho ya Sherehe za Uhuru ili fedha ambazo zingetumika zielekezwe kwenye miradi ya maendeleo na vile vile imeelekeza kuhakikisha azma ya kuhamishia Makao Makuu ya Serikali Dodoma inatimizwa. 

Majukumu yote niliyoyataja yanategemea Mapato ya Serikali.  Vile vile gharama za kuendesha Michezo ya SHIMIWI kwa kiasi kikubwa zinatokana na Bajeti ya Serikali.  Tunapenda kuwaarifu Wananchi, Wanamichezo wote na Watumishi wa Umma wote kuwa kwa kuzingatia majukumu yote ambayo Taifa inayatekeleza kwa sasa SHIMIWI imeamua kuunga mkono kwa kuahirisha michezo ya SHIMIWI  kwa mwaka huu 2016 ili kushirikiana kuelekeza nguvu pamoja na makundi mengine ya kijamii wakiwemo Watumishi wa Umma katika kutekeleza majukumu hayo.  Tunawashauri watumishi wote waendelee kufanya mazoezi kwa ajili ya kujenga afya zao kupitia ushiriki wa pamoja kwenye Bonanza la Wafanyakazi wa Umma katika maeneo yao katika siku za mwisho wa wiki.

Vile vile naomba nitumie fursa hii kusisitiza vilabu wanachama vihakikishe vinalipa ada ya mwaka kwa ajili ya maandalizi ya Mkutano Mkuu wa mwaka utakaofanyika Januari, 2017.  Hadi sasa ni timu chache zimekwishalipa.  Kumbukeni kwamba kwa mujibu wa katiba ya SHIMIWI wanachama watakaoshiriki kwenye Mkutano Mkuu wa mwaka ni wale waliolipa ada ya mwaka.  

Daniel Mwalusamba.
MWENYEKITI - SHIMIWI - TAIFA
11 Oktoba, 2016
KWA PAMOJA MAKUNDI YOTE YA KIJAMII
TUSHIRIKIANE KULIJENGA TAIFA LETU TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA MUNGU IBARIKI TANZANIA.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...