Benny Mwaipaja,
MoFP
Washington DC,
Marekani
8.10.2016
WAZIRI wa Fedha na
Mipango, Dkt. Philip Mpango, amesema kuwa Serikali imedhamiria kuimarisha sekta
ya kilimo na Utalii ili ziweze kutoa mchango mkubwa kuinua uchumi wa Taifa
pamoja na kuwaondoa wananchi wake kutoka katika lindi la umasikini.
Waziri Mpango
ameyasema hayo Jijini Washington DC, nchini Marekani, wakati akizungumza na
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis
Rene Peter Larose, ambapo viongozi hao wamezungumzia masuala yanayohusu
utekelezaji wa miradi mbalimbali inayofadhiliwa na taasisi hiyo.
Amesema kuwa
kilimo kinaajiri asilimia kubwa ya watanzania hivyo mapinduzi yanayokusudiwa
katika sekta hiyo ni kuendesha kilimo biashara kwa kuongeza uzalishaji na thamani ya mazao ya wakulima.
Kuhusu sekta ya
Utalii, Dkt. Philip Mpango anayeongoza ujumbe wa wataalamu wa Uchumi na Fedha
katika Mkutano wa Mwaka ulioandaliwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha
Duniani, IMF, amesema kuwa serikali inakusudia kupitia upya kodi zinazoleta
kero mbalimbali katika sekta hiyo pamoja kilimo.
Eneo jingine
alilotaka Benki ya Dunia kuingilia kati, ni kuipatia Tanzania Mkopo na ruzuku
utakaosaidia kukabiliana na madeni yake makubwa inayodaiwa na Mifuko ya Hifadhi
ya Jamii pamoja madeni ya Shirika la Ugavi wa Umeme nchini, TANESCO, ili
shirika hilo liweze kujiendesha kwa faida na kuchangia ukuaji wa uchumi wa
Taifa kwa haraka.
Kwa Upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis
Rene Peter Larose, ameihakikishia Tanzania kuwa pamoja na miradi mingine,
itafadhili mradi mkubwa wa kilimo wa ukanda wa kusini “Southern Agricultural Growth Corridor of Tanzania (SAGCOT)” ili kukifanya kilimo kuwa na tija kwa wananchi na
taifa kwa ujumla.
“Mimi
nimefika Tanzania na ninaifananisha nchi hiyo kuwa itafikia ama kuzidi hadhi ya
Dubai kutokana na rasilimali nyingi ilizonazo ambazo zikisimamiwa vizuri
zitaibadili kabisa nchi hiyo kimaendeleo” alisema Larose.
Ameitaka
Tanzania kutosita kuitumia ipasavyo benki hiyo kufanikisha malengo yake ya
maendeleo na kwamba yeye mwenyewe binafsi pamoja na kwamba anaongoza kundi la
nchi 22 za kiafrika katika Benki hiyo, atahakikisha Tanzania kama zilivyo nchi
nyingine, inanufaika na uwepo wa Taasisi hiyo.
Mkurugenzi
huyo Mtendaji amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli, namna anavyosimamia mambo kwa nguvu zake zote na ametoa pole kwa nchi
hiyo kutokana na madhara iliyoyapata kufuatia tetemeko kubwa la ardhi
lililoukumba mkoa wa Kagera na mikoa mingine jirani.
Ameahidi
kuwa Benki hiyo itatuma wataalamu watakaosaidia kufanya utafiti na kuishauri
nchi kitaalamu na kimiundombinu namna ya kukabiliana na majanga ya matetemeko
pamoja na vifaa vitakavyosaidia kutoa tahadhari kabla ya kutokea kwa majanga
kama hayo.
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango (kulia) akisalimiana na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya Dunia anayeshughulikia Kanda ya Afrika, Louis Rene Peter Larose walipokutana ofisini kwake Jijini Washington DC, Marekani, ambapo wamezungumzia masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya Tanzania na namna Benki hiyo ilivyojipanga kuhakikisha kuwa inaiwezesha Tanzania kufikia ndoto yake ya kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025
Serikali imekopa ktk mifuko ya kijamii. Imeshindwa kulipa hivyo inaomba mkopo benki ya dunia ili kulipa deni lake ktk mifuko ya kijamii.
ReplyDeleteSerikali pia inaomba mkopo kulipa madeni ya tanesco. Hawa tanesco wanatumia kiasi gani kuwalipa IPTL? Hivi kwanini serikali haitatui suala la IPTL once and for all?