Na. Immaculate Makilika- MAELEZO

Serikali ya Tanzania na Cuba zimeahidi kuendeleza ushirikiano uliopo, ambao umeasisiwa na viongozi wa mataifa hayo Mwalimu Julius Kambarage Nyerere wa Tanzania pamoja na Fidel Castro Rais mstaafu wa Cuba.

Akizungumza na waandishi wa habari, Ikulu leo jijini Dar es salaam, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu, amesema kuwa Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Valdes Mesa ameitikia mwaliko huo wa kuja nchini kwa vile nchi hizo mbili zimekua na ushirikiano na mahusiano mazuri kwa muda mrefu.

“Ziara hii ni moja ya jitihada za Serikali hizi mbili ya Cuba na Tanzania katika kuendelea kuimarisha na kudumisha mahusiano mazuri yaliyopo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili ili kuhakikisha mahusiano yaliyopo yanaimarika zaidi” alisema Makamu wa Rais

Katika ziara hiyo ya Makamu wa Rais wa Cuba nchini, mambo mbalimbali yalijadiliwa ikiwemo masuala ya Afya, Elimu, Michezo, na Utamaduni, ambapo katika sekta ya afya nchi ya Cuba imepiga hatua na kuahidi kushirikiana na Tanzania ili kujenga kiwanda cha kisasa cha kutengeneza madawa ya binadamu.

Aliongeza kuwa Tanzania imeomba Serikali ya |Cuba kuendelea kusaidia sekta hiyo kwa kufundisha wataalamu wa afya, ambapo tayari madaktari 24 kutoka Cuba wako nchini kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma za kitabibu na mafunzo katika mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara na Visiwani.

Masuala mengine yaliyojadiliwa katika ziara hiyo ni pamoja na ushirikiano katika sekta ya elimu, biashara, utalii na uwekezaji.Ambapo pia Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Suluhu amesisitiza nia ya Serikali ya Tanzania kudumisha ushirikiano huo ikiwa ni pamoja kupongeza jitihada za kuboresha uhusiano wa Cuba na Marekani.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Cuba, Mhe. Salvador Antonio Valdes Mesa ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuendelea kuonesha ushirikiano kwa nchi yake na kuahidi kuendelea kutoa msaada kwa Tanzania.“Tumeamua kuendelea kuboresha mahusiano yetu na Tanzania kwa kuongeza ushirikiano wetu katika sekta nyingine ambazo hatukuwa tunashirikiana hapo awali kama vile sekta ya utalii” alisema Makamu wa Rais wa Cuba

Aidha, Mhe. Mesa ameiomba Tanzania kuendelea kuiunga mkono Cuba katika masuala ya kimataifa ili kuendeleza ushirikiano na kukuza uchumi kwa nchi zote mbili.

Makamu wa Rais wa Cuba aliwasili nchini jana jioni kwa ziara ya siku tatu ambapo alipata fursa ya kuonana na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa John Magufuli .
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Mgeni wake Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa wakati alipokutana naye Ikuu leo kwa mazungumzo ambapo wamezungumzia jitihada za Serikali hizi mbili ya Cuba na Tanzania katika kuendelea kuimarisha na kudumisha mahusiano mazuri yaliyopo kwa manufaa ya wananchi wa nchi hizi mbili.(PICHA KWA HISANI YA OFISI YA MAKAMU WA RAIS)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan na Mgeni wake Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Tanzania na Cuba.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akimkabidhi zawadi ya picha ya mnyama Chui anayepatikana katika mbuga za wanyama za Tanzania Mgeni wake Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea zawadi ya picha kutoka kwa Mgeni wake Makamu wa Rais wa Cuba Mh. Salvador Valdes Mesa , Kulia ni Mhe. Balozi Dkt. Augustine Mahiga Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kikanda na Kimataifa.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...