Nteghenjwa Hosseah - Arusha

Wananchi wa Kata Pinyinyi, Wilaya ya Ngorongoro wanasumbuliwa na ugonjwa wa ajabu wa kutapika damu kwa takribani miaka minne sasa na hali hii imewasababisha wananchi hao kuwa na hofu na kukosa amani ya kuendelea kuishi katika makazi yao.

Wakiwasilisha kero zao mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Mrisho Gambo ambaye yuko katika ziara ya Kikazi kwenye Wilaya hiyo wananchi hao wamesema mpaka sasa wananchi zaidi za ishirini wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo ambao mpaka sasa hawafahamu kwamba ni ugonjwa gani.

“Ugonjwa huu ulianza tangu 2012 na mgonjwa huwa anatapika damu kwa kipindi kirefu na baadae hufariki na sisi kama wananchi wa Kijiji hiki tulishapeleka taarifa hizi kwa Halmashauri ya Wilaya na wakaja mpaka hapa kijijini lakini ufumbuzi wa ugonjwa huu haujapatikana kutokana na kutokua na majibu sahihi ya chanzo na aina ya ugonjwa huu” alisema Zakayo Siranga mkazi wa Punyinyi.

Aliongeza kwa kusema kuwa wagonjwa wa aina hii wakienda kutibiwa katika Hospital zetu hawaponi lakini kuna wachache waliokwenda Nchi jirani ya Kenya kupata matibabu walipona sasa hatuelewi nini ambacho kimeshindikana katika Hospital zetu tunaomba Serikali itusaidie.

Akijibu hoja hiyo Mganga Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro Dr. Omary Sukari amethibitisha kuwepo kwa ugonjwa huu na alieleza jitihada ambazo zimefanyika kutafuta ufumbuzi wa ugonjwa huu na kuwa wamekwisha chukua sampuli ya damu na kupeleka kwenye Taasisi ya Utafiti Magonjwa wa magonjwa ya Binadamu(NIMR) lakini mpaka sasa hawajapata majibu kutoka katika Taasisi hiyo.

Rc Gambo alimuagiza Mganga Mkuu wa Mkoa Dr. Frida Motiki kutuma wataalamu ndani ya wiki hii wa kufanya tafiti ya ugonjwa huo hatari na kupeleka tena sampuli hiyo NIMRI ili kupata taarifa sahihi na kutafuta ufumbuzi wa haraka.

“Ugonjwa huu ni hatari sana na sisi kama Serikali hatuwezi kukaa Kimya kwa sababu unagharimu uhai wa watu, kwa takwimu hiyo ya watu 21 kufariki ni kitu cha kusikitisha sana hivyo nahitaji kupata ufumbuzi wa ugonjwa huu kupitia kwa wataalamu wangu wa Afya”.

Kata ya Pinyinyi haijawahi kutembelewa na Kiongozi wa Ngazi ya Mkoa kwa zaidi ya miaka kumi sasa wananchi hao walitoa shukrani zao kwa Mkuu wa Mkoa Mhe. Gambo kwa kuanzia ziara yake katika Kata hiyo na kueleza kwamba wanaona sasa wao ni sehemu ya wananchi halali wa Mkoa huu kwa kuwa walikua wamesahaulika kwa kipindi kirufu na wana imani kero zao sasa zitapata ufumbuzi wa haraka.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha (kwanza kulia) akitoa maelekezo wakati anakagua ujenzi wa madarasa manne katika Shule ya Sekondari Lake Natron iliyopo Wilayani Ngorongoro. Rc alizidi kuwapongeza kwa usimamiaji makini wa mradi huo.
Rc Gambo akiongea na wananchi wa Kijiji cha Pinyinyi kwenye Mkutano wa hadhara. Wananchi hao wameomba msaada wa haraka kwa tafiti na tiba ya ugonjwa wa ajabu unaowasumbua wa kutapika Damu na mpaka sasa umesababisha vifo 21.
Hawa ni wananchi wa Kata ya Digodigo (wazee) ambao Mkuu wa Mkoa wa Arusha ametoa Fedha kwa ajili ya kujiunga na huduma ya Tiba kwa Kadi (Tika) chini Mfuko wa Bima ya Afya. Rc aliendesha zoezi la kuhamasisha wananchi kujiunga na kila aliyeambatana naye kwenye Msafara wake alimtaka kuchangia wananchi 2-6 kujiunga na Tiba kwa Kadi. Idadi ya Kaya 127 zimefanikiwa kujiunga na Tika kupitia zoezi hili.

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...