Na Lulu Mussa -Kasulu 

Imebainika kuwa ongezeko kubwa la idadi ya wakimbizi katika kambi ya Nyarugusu inachangia kwa kiasi kubwa la uharibifu wa mazingira kwa kuongeza matumizi ya rasilimali za asili. 

Hayo yamesemwa leo na Kaimu Mkuu wa Kambi ya Nyarugusu Bw. Peter Bulugu wakati wa kuwasilisha taarifa ya hali mazingira katika kambi hiyo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba.
 
Kaimu Mkuu wa Kambi wa Nyarugusu Bw. Peter Bulugu amesema kuwa hali ya mazingira katika kambi si nzuri na inakabiliwa na tatizo la uharibufu wa mazingira kwakuwa wengi wa wakimbizi hao hutumia kuni kama nishati ya kupikia. 

Hata hivyo Bw. Bulugu amebainisha kuwa Ofisi yake imeeanda mkakati wa upandaji miti ili kunusuru maeneo yanayozunguka, na kwakuanzia jumla ya miche 900,000 imeoteshwa katika vitalu. Pia Kambi imedhamiria kugawa majiko banifu ambayo yatatumia nishati kidogo na uzalishaji wa nishati kwa kutumia takataka za mashambani unatarajiwa kuanza mwezi Novemba. 

Aidha, mkakati mwingine ni ujenzi wa nyumba za tofali mbichi na kuezeka kwa mabati badala ya miti ambapo jumla ya nyumba 800 zimekamilika na nyumba 542 ziko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Alisema Bw. Bulugu.
 
Akiwa katika Wilaya ya Kasulu Mkoani Kigoma, Waziri Makamba ametembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu na kupata fursa ya kuongea na wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma katika kambi hiyo. 

Waziri Makamba amesema kuwa ni vema uongozi na mashirika yanayotoa misaada katika kambi hiyo kuandaa mpango mzuri wa namna ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi ili ujio wao usiathiri watanzania wanaozunguka kambi ili shughuli zao za uzalishaji mali kila siku ziwe na tija.
  
Waziri Makamba aliuagiza Ungozi wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalohusika na wakimbizi kutafuta pesa zaidi ili mpango wa kugawa majiko banifu uwafikie wakimbizi wote. “Kaya zilizopo hapa ni 30,000 ninyi mnataka kugawa majiko hayo kwa kaya 3000 tu, nashauri muangalie uwezekano wa kugawa kwa kaya zote” Makamba alisisitiza. 

Waziri Makamba pia ameagiza kufanyika kwa Ukaguzi wa Mazingira (Environment Audit) ndani ya wiki mbili kwakuwa ni takwa la kisheria. Na kuwataka na kupanda miti kwa wingi. ” Pandeni miti ya aina mbalimbali mfao miti ya matunda, kuni na mbao ili kunusuru mazingira yetu”. 

Waziri Makamba pia alitembelea msitu wa Makere wenye takriban ekari 75,000 ambao kwa upande wa Makere kusini kumekuwa na uharibufu mkubwa wa mazingira na kuagiza doria za mara kwa mara ili kudhibiti wananchi wanaofanya kilimo cha kuhamahama, kukata na kuchoma miti pia kudhibiti ongezeko la mifugo kwa kuiandikisha ili mgogoro uliopo baina ya hifadhi na wananchi uweze kupatiwa ufumbuzi kwa kujenga hoja madhubuti. 

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia masuala ya Muungano na Mazingira Mhe. January Makamba hii leo ameendelea na ziara ya kukagua hali ya mazingira katika Mikoa 10 hapa nchini ambapo leo ni siku ya 13. Waziri Makamba pia atatembelea Mkoa wa Tabora.
Mbunge wa Kasulu vijijini Mhe Augustine Vuma (Kushoto) akitoa maelezo kwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba wakati viongozi hao walipotembelea kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu. (Katikati ni Bw. Peter Bulugu Kaimu Mkuu wa Kambi – Nyarugusu
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akihutubia katika Mkutano wa hadhara katika Kijiji cha Kagera Nkanda, Wilayani Kasulu
Sehemu ya wawakilishi wa mashirika mbalimbali yanayotoa huduma katika kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba (hayupo pichani) mara baada ya kutembelea kutembelea kambi ya Nyarugusu na kutoa maelezo katika sekta ya mazingira
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. January Makamba akiwa na Mkuu wa Wilaya ya Kasulu Kanali Martin Mkisi wakikagua uharibifu wa mazingira katika msitu wa Makere katika Wilaya ya Kasulu .

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...