* Aagiza Halmashauri kuwapatia mikopo wanawake wajasiriamali waliopo stand ya Kabwe.* Awataka wazazi na walezi kuhakikisha wanasimamia malezi ya watoto wao.

Na Erasto Ching’oro- Msemaji wa Wizara, Mbeya

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy Mwalimu (Mb.) amefanya ziara ya kushtukiza katika Stendi ya Kabwe Jijini Mbeya kwa ajili ya kuongea na wanawake wajasiriamali wanaofanya biashara katika stendi hiyo ili kufuatilia utekelezaji wa Ilani kuhusu Halmashauri kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. Akiongea na Wanawake hao Waziri Ummy Mwalimu amewataka kujiunga katika vikundi ili kuwawezesha kukopesheka na kupata fursa mbalimbali za biashara ikiwemo mafunzo na masoko.

Mhe. Ummy, alieleza kuwa Serikali itahakikisha inawapa mikopo yenye riba nafuu kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, na pia kuweka mazingira wezeshi ya kuwajengea uwezo wa kufanya biashara zao katika mazingira salama. Hivyo amewasisitizia kuwa ni muhimu wajiunge katika vikundi ili waweze kufikiwa na fursa za huduma za masoko na mikopo kwa kwa wepesi zaidi. 

Kwa upande wao, wanawake wajasiriamali hao katika stendi ya Kabwe walisema changamoto kubwa waliyonayo ni kukosa mitaji na masoko hali ambayo ilimlazimu Waziri Ummy kumuagiza Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya kuhakikisha anawapatia mikopo wanawake wa Standi ya Kabwe ndani ya mwaka huu wa fedha wa 2016/17.

Pia akiwa katika soko hilo, Waziri Ummy ameeleza kufurahishwa na jitihada za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Amos Makalla na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Mhe William Paul Ntinika kwa kuwahamasisha wajasiriamali hao kufanya biashara zao katika mazingira ya usafi kwa kufanikisha matumizi ya meza za kufanyia biashara katika eneo hilo. Mhe. 

Waziri Ummy alitoa rai kwa Halmashauri nyingine kuiga mpango wa kufanya biashara katika mazingira ya usafi ili kuhakikisha tunadumisha usafi wa miji yetu na mazingira ya maeneo ya wafanyabiashara wadogowadogo. 

Aidha, akiwa Mkoani Mbeya Waziri Ummy alitembelea Mahabusu ya Watoto iliyopo katika Jiji la Mbeya. Akiongea na watoto takribani 16 waliopo katika Mahabusu hiyo Waziri alieleza kuwa Serikali itahakikisha watoto waliopo mahabusu wanapata haki zao zote za msingi hususan haki ya kupata elimu kwa maendeleo na ustawi wao. 

Hata hivyo, Waziri Ummy ametoa rai kwa wazazi na walezi wa watoto wote nchini kuhakikisha wanawalea watoto wao katika misingi bora itakayo wawezesha kuwa na tabia njema. Hii itasaidia kupunguza idadi ya watoto wanaokinzana na sheria na kupelekea kufikishwa katika mahabusu za watoto. 

Waziri alionya kuwa makosa mengi yanayowakumba watoto waliopo mahabusu msingi wake mkubwa ni malezi mabaya yanayo pelekea watoto kukosa maadili ambayo hujikuta wamehusishwa na makosa ya mauaji, wizi, ubakaji na ulawiti. Hivyo kila mzazi ano wajibu wa kulea watoto katika maadili na tabia njema ili kuepuka migogoro ya kisheria. 

Aidha, Watoto hao waliopo mahabusu ya watoto Mbeya walimuomba Waziri Ummy kusaidia kuharakisha kusikilizwa kwa mashauri ya kesi zinazowakabili zilizopo mahakamani ili waweze kurudi nyumbani, wakiwa huru na kuendelea na masomo.

Waziri Ummy yupo Mkoani Mbeya kwa ziara ya Kazi ya siku 2 ambapo pia tarehe 01 Oktoba 2016 atakuwa Mgeni Rasmi kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yanayofanyika kitaifa eneo la Rujewa, Wilayani Mbarali.

 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akikagua usafi wa eneo la soko la wanawake wajasiriamali, alipofanya ziara ya kushitukiza katika soko lililoko Stendi ya Kabwe Jijini Mbeya tarehe 30/9/2016. 
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akiongea na wanawake wajasiriamali, alipofanya ziara ya kushitukiza katika soko lililoko Stendi ya Kabwe Jijini Mbeya ili kufuatilia utekelezaji wa Halmashauri kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. (30/9/2016)
 Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Ummy A. Mwalimu (Mb.) akiongea na wanawake wajasiriamali, alipofanya ziara ya kushitukiza katika soko lililoko Stendi ya Kabwe Jijini Mbeya ili kufuatilia utekelezaji wa Halmashauri kutenga asilimia 5 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake. 

Michuzi Blog

Tanzanian blog operating since 2005, covering International news and Local News, including Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers.

Toa Maoni Yako:

0 comments so far,add yours

Hii ni Blog ya Watanzania popote walipo duniani kwa ajili ya kuhabarisha, kutoa/kupokea taarifa na kuelimisha mambo yote yaliyo chanya kwa Taifa letu. Tafadhali sana unapotoa maoni usichafue hali ya hewa wala usijeruhi hisia za mtu/watu. Kuwa mstaarabu...